UFUNGUZI WA KIKAO CHA KAMATI YA AFYA YA MSINGI (PHC) MKOA CHA KUJADILI ZOEZI LA KITAIFA LA UTOAJI WA DOZI MOJA YA CHANJO YA KUZUIA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI (HPV) KWA WASICHANA WENYE UMRI WA MIAKA 9-14
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi Mwanahamis Munkunda mapema leo hii ameongoza kikao cha ufunguzi cha kamati ya Afya ya Msingi (PHC) Mkoa ambapo ameanza kwa kusema, nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutuleta pamoja katika kikao hiki. Pili, napenda kuwakaribisha wajumbe wote katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ya Mkoa (PHC) kilichoandaliwa rasmi kupeana taarifa na kujadili mikakati ya utakelezaji wa zoezi la kitaifa la utoaji wa dozi moja ya chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 9-14 litakalofanyika nchi nzima kuanzia tarehe 22 hadi 26 Aprili, 2024.
Bi Munkunda akaendelea kusema, ni dhahiri kwamba chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi ijulikanayo kitaalamu kama “Human Papilloma Virus-HPV” ndio mkakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na saratani ya mlango wa kizazi, hivyo kupunguza gharama kubwa za matibabu kwa familia zetu na Taifa kwa ujumla.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) hupendekeza chanjo ya HPV kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 9-14. Aidha, hapo awali Tanzania kupitia Wizara ya Afya ilichagua kutoa dozi mbili za chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 pekee. Chanjo hii imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2018 na zoezi hili limekuwa likifanywa na Halmashauri zetu kwa kushirikiana na Mkoa, OR-TAMISEMI, Wizara ya Afya na wadau mbalimbali kupitia vituo vya kutolea huduma za afya.
Kaimu Mkuu wa Mkoa akaendelea kusema, Nimefahamishwa kwamba zoezi lenye kuleta mabadiliko ya kutoa dozi moja ya chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 9-14 litafanyika nchini kuanzia tarehe 22 hadi 26 Aprili 2024. Kupitia zoezi hili, Mkoa wetu unatakiwa kuwafikia wasichana wapatao 119,796. Uzoefu wa mazoezi yaliyotangulia unaonesha kwamba mara zote tumevuka malengo tuliyojiwekea kwani idadi hii ni makisio tu na siyo idadi kamili ya walengwa wote waliopo kwenye jamii.
Munkunda akasisitiza kuwa, zoezi hii litafanyika kupitia shule za msingi na sekondari kwani walengwa wengi hupatikana shuleni, na kupitia vituo maalumu vilivyoandaliwa mitaani kwa ajili ya wasichana waliopo nje ya mfumo wa shule.
Akamalizia kwa kutoa wito kwa viongozi wote katika Mkoa, kuhakikisha wanapeleka ujumbe kwa jamii kuhusu kufanyika kwa zoezi hili ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha na kuwaelekeza wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu wanaotekeleza zoezi hili muhimu. Chanjo hizi ni salama, hazina madhara yoyote, zimethibitishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Aprili 19, 2024
Wizara ya Afya Tanzania
World Health Organization (WHO)
#TunaifunguaMtwara
#KaziIendelee
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.