Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego akikata utepe kuashiria ufunguzi wa kabati za kuhifadhia vifaa vya maabara Shule ya Sekondari Mikangaula wakati ziara yake inayoendelea wilayani hapa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu katika kutatua changamoto za Elimu. Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya kikazi inayoendelea hapa Wilayani Nanyumbu amesema uongozi wa Wilaya ya Nanyumbu ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mheshimiwa Joackim Wangabo pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hamis Dambaya umemkabidhi mpango mkakati ambao unatekelezeka kwa vitendo.
Amesema kwa muda mrefu wilaya ya Nanyumbu imekuwa ikinyooshewa vidole kwa kuwa na matokeo mabaya ya mitihani kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari. Amesema mpango mkakati aliokabidhiwa na hali halisi anayoiona kwa vitendo ni ushahidi tosha kwamba Nanyumbu sasa inakimbia katika maendeleo.
Amesema kwa muda mrefu vyombo vya habari akiwemo ‘Mwewe’ wa Cloudz TV wamekuwa wakitembelea na kuripoti changamoto nyingi za wilaya hii. Amesema ni jambo jema kwani linawaamusha na kuwakumbusha kutimiza wajibu wao. Aidha, amemtaka Mwewe arudi Nanyumbu ili kujionea mabadiliko yaliyopo sasa.
Hata hivyo Mheshimiwa Dendego amesikitishwa na mimba za wanafunzi na kutangaza mapambano makubwa na wanafunzi wanaopata ujauzito. Amesema taarifa zinaonesha mwaka 2016 jumla ya wanafunzi 22 wilayani Nanyumbu walipata ujauzito. Amesisitiza kuwa suala hilo halikubaliki kwani linadumaza maendeleo.
Amesema mwanafunzi anayepata ujauzito ni mtuhumiwa namba moja. Aidha amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha anamfikisha kwenye vyombo vya sheria mwanafunzi yeyote anayepata ujauzito shuleni. Amesema watoto wa kike wamekuwa sababu mojawapo ya ushawishi wa kupata mimba kwa kuvaa nguo zinazoshawishi zinaa, pia vitendo vya kuwavutia wavulana.
Amesema maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais ya kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi shule kwa mfumo wa kawaida ni sahihi na yeye mwenyewe yuko tayari kuyasimamia. Amewataka wananchi na makundi ya kijamii yanayopiga kelele kupinga hatua hiyo yaache mara moja.
Licha ya kuwataka wanafunzi wa Nanyumbu kubadilika Mheshimiwa Dendego ametoa michango mbalimbali katika sekta ya Elimu ambapo amechangia mifuko ya saruji 50 katika shule ya Msingi Lidede na kuahidi kugharamia mbao za milango na madilirisha katika shule hiyo.
Awali akiwasilisha mpango mkakati wa Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Hiyo, Hamis Dambaya amesema kuwa kwa kutambua changamoto kubwa ya elimu katika halmashauri hii wameamua na wamejipanga katika miakakati imara inayotekelezeaka.
Moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwatumia wananchi ambao wamehamasika na kuitambua falsafa ya uchangiaji wa elimu. Amesema kutokana na uhaba wa fedha katika utekelezaji wa malengo waliojiwekea wananchi wamehamasika kutumia nguvu zao katika kufyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo. Aidha katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Halmashauri imetenga shilingin 250,000,000 kupitia fedha za maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule za msingi Mikuva, Michiga B, Nanderu, Nandete na Nakatete. Kwa sasa wilaya hiyo ina upungufu wa vyumba vya madarasa 254 sawa na asilimia 50. Wakati ujenzi wa nyumba za walimu umefikia asilia 63.
Mikakati mingine ni kuongeza uwezo wa idara ya Uthibiti wa ubora wa elimu katika kukagua shule ambapo wamekuwa wakisaidia kwa huduma ndogondogo ikiwemo usafiri kuzifikia shule husika.
Kwa upande wa wananchi wa Nanyumbu wamepongeza Mheshimiwa Dendego kwa kuthamini jitihada zao na kumtaka aendelee kuwabana wazazi wasiojiheshimu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mikangaula, Said Mkareha amemtaka Mheshimiwa Dendego aendelee kupambana. Pia awabane wazazi wanaovaa nguo zisizo stahili kwani ni moja ya vishawishi vya zinaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.