Kamati ya siasa mkoa wa Mtwara ikiongozwa na Ndg. Mobutu Malima, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara, leo tarehe 07 Novemba 2024 wametembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji Nanyamba pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Mtwara inayotekelezwa kwa Ilani ya chama hiko.
Katika ziara hiyo, Ndg. Malima amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba kuhakikisha huduma za maji na umeme zinafika katika Zahanati ya kijiji cha Milangominne ambayo tayari imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD).
Aidha, Ndg. Malima ametoa rai kwa viongozi wa CCM ngazi ya vijiji kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa walimu wanaopangiwa kufundisha katika maeneo yao huku akiwataka waendelee kuweka mkazo kwa wazazi kuwapeleka watoto shule.
“Naomba muwakubali walimu, diwani panga ratiba yako uwe unafika kuwasilikiza walimu kujua changamoto zao, tunahitaji tupate matokeo chanya kwa watoto wetu, wapeni ushirikiano wajione ni sehemu ya jamii” Aliendelea kueleza Ndg. Malima.
Miradi nane yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 2 imetembelewa na Kamati hiyo, ikiwemo Shule ya Msingi Chawi, Zahanati ya kijiji cha Milangominne, mradi wa maji Njengwa, Shule ya Sekondari Dinyecha, Shule ya msingi ufundi na elimu maalum Nanguruwe, Shule ya msingi Nambeleketela, Shule ya msingi Ziwani, Shule ya Sekondari Nalingu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.