Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda (mwenye suti nyeusi) akipokea msaada wa vitabu toka kwa Mwakilishi wa kampuni ya Ndovu Resources LTD, James Chialo. Anayefuata kutoka kushoto ni Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Kanuda Nswira. Kaimu Mkurugenzi Mkurugenzi Manispaa ya Mtwara Mikindani, Sambwe Sijabaje. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya Mtwara, George Mrisho. (Picha na Jamad Omari, Afisa Habari Manispaa ya Mtwara Mikindani)
Kampuni ya Ndovu Resources LTD inayoshughulika na utafiti wa mafuta na gesi asilia mkoani Mtwara imetumia shilingi milioni 720 kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo mkoani hapa. Misaada hiyo imekuwa ikitolewa katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ya ujenzi.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda Wakati akipokea msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ligula pamoja na vitabu kwa ajili ya shule za mkoani Mtwara vilivyotolewa na kampuni hiyo.
Ametaja baadhi ya misaada ambayo kampuni hiyo imekuwa ikitoa kwa nyakati tofauti kuwa ni pamoja na gari la kisasa la kubebea wagonjwa, vitanda vya wagonjwa, vifaa tiba. Pia msaada wa saruji kwa ajili ya ujenzi wa kondo, vyote vikiwa vimetolewa kwa nyakati tofauti katika hospitali ya Nanguruwe iliyoko wilayani Mtwara.
Kwa upande wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Ligula mapema mwaka jana kampuni hiyo ilitoa msaada wa vitanda vya kisasa pamoja na vifaa tiba.
Aidha, Ndovu Resources wameweza kusaidia vitanda na magodoro ya wagonjwa kwa zahanati za Nkunwa, Chawi na Mbawala zilizoko mkoani Mtwara.
Mheshimiwa Mmanda ameshukuru na kuwapongeza Ndovu Resources kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakijitolea kusaidia maendeleo na kutatua changamoto nyingi za mkoa wa Mtwara.
Akikabidhi msaada wa vifaa tiba na vitabu vya ziada kwa kaimu Mkuu wa Mkoa, mwakilishi wa kampuni hiyo, James Chialo amesema Ndovu wana wajibu wa kusaidia jamii katika maeneo wanayofanya kazi hivyo wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha jamii inanufaika na uwekezaji wao. Licha ya msaa huo, wako katika mchakato wa kutoa huduma ya maji kwa vijiji vya Namayakati shuleni na Namayakati barabarani vilivyoko Wilayani Mtwara.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanuda Nswila amewashukuru Ndovu Resource na kuwataka wadau wengine kuiga mfano wao kwa kujari jamii inayowazunguka. Aidha amewataka Ndovu Resources LTD kuwa na utamaduni wa kuweka nembo ya kutambulisha misaada yao mingi ambayo wamekuwa wakitoa ili iwe alama ya utambulisho kwa mazuri wanayoyafanya.
Kampuni ya Ndovu ilipata leseni ya kufanya utafiti katika mikoa ya Lindi na Mtwara mwaka 1999. Hadi sasa wameshafanya utaafiti na uchimbaji katika maeneo ya Songosongo na Nyuni mkoani Lindi, pia Likonde, Ntorya1 na Ntolya 2 katika mkoa wa Mtwara.
kutazama video ya tukio zima bonyeza HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.