Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Joseph aakizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mtwara wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara
Wakazi wa mkoa wa wa Mtwara wanatarajia kunufaika na mpango wa utoaji wa vitambulisho vya taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). Mpango huu unaotarajiwa kuanza Novemba 13, mwaka huu unakusudia kuwafikia wakazi zaidi ya 1,121,663 walioko mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliofanyika katika ukumbi wa Boma Mkoa ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara jana, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Joseph amesema zoezi hili litaanza Novemba, 13 mwezi huu na kwamba kufikia Februali 2018 wanatarajia kuwa wamekamilisha kuandikisha wananchi wote na hatimaye kutoa namba za vitambulishio wakati vitambulisho vikiendelea kuzalishwa.
Anasema zoezi hili linakuja kwa mara ya pili baada ya kukamilika kwa zoezi la awali lililowahusisha watumishi wa Umma lililofanyika mapema mwaka huu. Aidha mwaka 2014 kulifanyika zoezi la kuandikisha wananchi ambapo hatua za ujazaji wa fomu ulifanyika.
Amewataka wale waliojiandikisha mwaka 2014 katika zoezi lililofanyika nchi nzima kujitokeza katika vituo vya kuandikisha ili kupata maelekezo yatakayowezesha taaifa zao kuingizwa katika mfumo wa sasa wa kielektloniki.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda aliyekuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Gelasius Byakanwa amewataka wananchi wa kuchangamkia fursa hiyo kwani ni muhimu kwa maendeleo yao.
Amesema kitambulisho cha Taifa kitawawezesha wananchi kupata fursa mbalimbali kama vile ajira, nafasi za uongozi, Afya, uchumi na mengine mengi.
Amewataka wakuu wa wilaya wote, wakurugenzi, Makatibu Tawala wa Wilaya, Viongozi wa Dini, wahakikishe wanasimamia zoezi hili kwa weledi ili kuhakikisha linafanikiwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda amewataka wakurugenzi na viongozi wote wa Mkoa kutoa ushirikiano ili kuepusha kasoro zitakazoweza kujitokeza. Amesema kwa jiografia ya mkoa wa Mtwara ulioko mpakani, kuna uwezeakano wa raia wa kigeni kujipenyeza ili kupata vitambulisho hivyo. Amewataka watu wote kuwa makini ili kuhakikisha kasoro hizo hazijitokezi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.