Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameitaka jamii kutofumbia macho watu wanaotekeleza ukatili wa kijinsia kwani kwa kufanya hivo ni kuchochea ongezeko la vitendo hivyo.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo leo katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Nanyamba Ufundi katika halmashauri ya Mji wa Nanyamba ambapo aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya.
Katika hotuba yake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Abbas amesema ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia ni jambo ambalo halikubaliki na hivo kuwataka wananchi katika ngazi zote kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi wanapowabaini wahusika.
Aidha katika hotuba hiyo ya Mkuu wa Mkoa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya iliongeza kuwa jitihada za serikali za kupambana na vitendo hivyo viovu zitafanikiwa endapo mapambano yataanzia katika ngazi ya familia, watu binafsi, shuleni, maofisini, katika nyumba za ibada, na pia katika majukwaa ya michezo.
Katika hotuba hiyo Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameonyesha kusikitishwa na ongezeko la vitendo vya ukatili kijinsia ambapo kuanzia Januari mpaka sasa takwimu zinaonyesha jumla ya watu 223 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia mkoani Mtwara, huku akiitaka jamii kupaza sauti juu ya wanaotekeleza vitendo hivyo kwa kutoa taarifa kwa vyombo vinavyotoa msaada wa kisheria.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Nanyamba Ufundi yakiwa na kauli mbiu "Kila uhai una thamani tokomeza mauaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto" ambayo yalihudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali pamoja na wakuu wa wilaya 5 za Mkoa wa Mtwara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.