Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala leo Novemba 27, 2024 majira ya Saa 2:00 asubuhi ameshiriki kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika kituo cha Shangani Mashariki Rest house ambapo amesema anaridhishwa na wasimamizi wanasimamia zoezi hilo .
Akizungumza na vyombo vya habari kituoni hapo alipokamilisha zoezi la kupiga kura, Kanali Sawala amesema yeye binafsi ametimiza haki yake ya kikatiba Kwa kumchagua Kiongozi katika eneo lake huku akitoa wito Kwa wanaMtwara wenye sifa kujitokeza kupiga kura ndani ya muda uliowekwa kisheria.
“Ndugu wanahabari bila shaka mmejionea jinsi wananchi walivyohamasika kushirika katika uchaguzi huu, Kwa ujumla zoezi linaendelea vizuri, utaratibu unafuatwa na amani imetawala” aliongeza Kanali Sawala.
Kwa upande wake msimamizi wa Kituo Cha Shangani Mashariki (Rest House) Bi. Ancilla Marembela amesema zoezi la kupiga kura limeanza ndani ya muda uliopangwa na linaendelea vizuri ambapo wapiga kura waliojiandikisha wanaendelea kujitokeza Kwa wingi kutimiza haki yao ya kikatiba.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Issa Juma Selemani amesema polisi imeimarisha doria katika vituo vyote 3734 vya kupigia kura na kuongeza kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri Kwa amani.
Wakazi wa Mkoa wa Mtwara wenye sifa waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura wanashiriki katika uchaguzi huo kuchagua viongozi wao akiwemo mwenyekiti wa Kijiji, Mwenyekiti wa mtaa, wajumbe wa kundi la wanawake pamoja na kundi mchanganyiko.
Zoezi la kupiga kura linatarajiwa kuhitimishwa leo majira ya 10:00 jioni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.