Korosho ni zao maarufu hapa nchini. Ni zao ambalo linatajwa kuingiza kiasi kikubwa cha fedha za kigeni hapa nchini. Thamani kubwa ya zao hilo imekuwa ikipatikana kupitia karanga yake ambayo inapatikana baada ya kubangua. Ziko taasisi nyingi ambazo zimekuwa zikijishughulisha na ugunduzi wa mazao mengine ambayo yanaweza kupatikana kutokana na zao hilo. Taasisi hizo ni pamoja na Chuo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI -Naliendele). Hawa wameweza kugundua maziwa yatokanyo na karanga ya korosho, juisi, siagi pamoja na mvinyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Kituo cha Naliendele (TARI-Naliendele), Dkt Fortunatus Kapinga
Wakati Naliendele wakiendelea na Tafiti zao, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa kawakumbuka wananchi wake anaowaongoza ambao wamekuwa wabunifu katika kuzalisha bidhaa mbalimbali kutokana na zao hilo. Bidhaa hizo ni pamoja na pombe ya Mabibo. Anachokusudia kukifanya Byakanwa ni kuboresha pombe hiyo ili iwe bidhaa halali kupitia taratibu za kawaida za sheria za nchi. Iwe bidhaa ambayo itasaidia kuinua pato la wakulima hao.
Kwa muda mrefu pombe ya Mabibo imekuwa ikitengenezwa na kunyweka kwa siri na watu wa hadhi ya chini na kwa gharama ndogo. Maboresho ya Byakanwa yanakusudia bidhaa hii ianze kutengenezwa kwa njia halali na kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Ianze kunyweka na watu wa aina zote kama ambavyo konyagi na pombe zingine zimekuwa zikinyweka.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea wazalishaji wa pombe ya mabibo katika Kijiji cha Chigugu wilayani Masasi.
Byakanwa anaamini yote haya yanawezekana kutokana na utayari wa serikali ya awamu ya tano mbayo imejikita katika kuboresha Maisha ya watanzania. Pia kutokana na Msisitizo mkubwa wa serikali katika ujenzi wa viwanda. Wazo hili la Mheshimiwa Byakanwa linabebwa na Takwimu za uzalishaji wa bidhaa hiyo hapa Mkoani. Pia mazingira ya uzalishaji na nguvu kazi iliyopo.
Tukianza kwa kuzitazama takwimu, mkoa wa Mtwara unazalisha asilimia 65 ya korosho zote hapa nchini. Hili ndilo zao kuu la kibiashara katika mkoa huo likichukua asilimia 70.5 ya mazao yote ya biashara yanayolimwa Mkoani hapa. Kwa mjibu wa taarifa ya mkoa iliyowasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa Februali 20 mwaka huu, hadi tarehe hiyo mkoa ulikuwa umekusanya korosho tani 132,553. Huo ni uzalishji wa msimu mmoja tu wa mwaka 2019/2020.
Uzalishaji huo ukiuhusisha na tafiti za wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania kituo cha Naliendele, (TARI – Naliendele) yanaashiria uwezekano wa wazo la Mheshimiwa Byakanwa kuwa na tija kubwa. Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Fortunatus Kapinga anasema korosho ghafi inayosafirishwa na kubanguliwa ni asilimia 10 ya tunda zima ambalo huwa pamoja na bibo. Hiyo inamaanisha kwamba kwa mwaka 2019/2020 tayari tani 1,192,977 za mabibo zimetelekezwa huko mashambani. Haya ndiyo ambayo Byakanwa anataka yaingizwe katika viwanda, yatengeneze pombe, yaajiri wananchi, yaongeze kipato cha wananchi wa Mkoa wa Mtwara.
Byakanwa anasema wananchi wanahitaji kusaidiwa. kuongezewa maarifa na kuwezeshwa. Wawekewe mazingira ya uhuru katika uzalishaji.
“Mabibo hayohayo Naliendele wanayatumia kutengeneza mvinyo na Juice. Mwananchi wa kawaida aliyeyatumia kutengeneza pombe, tunamzuia. Mimi nimeona ni kufifisha kukua kwa viwanda na kuzuia kukua kwa ubunifu. Kama Mkuu wa Mkoa nataka kuwafikia hao wanaotengeneza pombe. Tuone wanatengenezaje. Bidhaa yao ya mwisho tuipeleke kwa watalaam kama ambavyo Naliendele wanapeleka TBS kupima. Mwisho tumwambie kinywaji chako ni halali. Aweze kukifikisha sokoni. Awe mlipaji kodi wa serikali. Aweze kuajili vijana wetu na tukitambuwe kama kiwanda”. Anasema Byakanwa.
Wazo hili lina changamoto nyingi ikiwemo hofu ya wananchi kukamatwa na vyombo vya dola. Hata hivyo Byakanwa anawatoa mashaka na kuwataka wajitokeze na kwamba ana nia njema.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa (wa tatu kutoka kulia) akifuatilia jinsi pombe ya mabibo inavyotengenezwa mara alipotembelea wazalishaji wa pombe hiyo katika Kijiji cha Chigugu wilayani Masasi.
Iwapo wazo hili litafanikiwa mnyororo wa thamani kwa zao la korosho utapanuka na kuchochea kilimo hicho. Kwa mkoa kama mtwara wenye kilometa za mraba 16,720 unalo eneo kubwa la kulima. Hali iko hivihivi kwa sehemu kubwa ya Tanzania. Tuombe utafiti huu mpya ufanikiwe kwani utawavusha siyo tu wanamtwara bali watanzania wote ambao wanashughulika na kilimo cha korosho.
Watanzania wengi wamekuwa wakitengeneza pombe kutokana na malighafi inayowazunguka. Iko mifano ya watu wengi ambao walisomeshwa kutokana na kinywaji cha pombe za kienyeji. Wazalishaji wa mhogo wanatengeneza kwa kutumia mhogo, wazalishaji wa ndizi wanatengeneza kwa kutumia ndivi. Hivyo kwa walio na mazao kama mahindi, Mtama, mianzi na nazi.
Tofauti na wengine ambao wanatumia mazao ya chakula kutengeneza pombe, Mabibo yamekuwa yakitelekezwa mashambani. Kuanza kuyatumia kwa uzalishaji wa bidhaa niyingine ni hatua kubwa ya kimaendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.