Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Elias Nyabusani akifungua mafunzo ya Mfumo wa Uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha ngazi ya kituo cha kutolea huduma (FFARS)
Mfumo wa Uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha ngazi ya kituo cha kutolea huduma (FFARS) umetajwa kuwa muarobaini wa matatizo mengi ya taarifa za matumizi ya fedha zikiwemo za Elimu bure. Kupitia mfumo huu fedha zote zinazotumwa ngazi ya vituo vya kutolea huduma kutoka serikalini zitakuwa zikionyeshwa katika mfumo mmoja ambao utamuwezesha mfuatiliaji kutambua kasoro kwa urahisi.
Mafunzo ya mfumo huu ambayo yanatolewa kwa udhamini wa watu wa Marekani kupitia mradi wake wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) kwa watendaji ngazi ya halmashauri hapa nchini unalenga kuondoa changamoto ya utoaji wa taarifa na utambuzi wa matumizi ya fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na serikali kwa watoa huduma kama vile shule, hospitali na zahanati hapa nchini.
Akizungumza na mwandishi wetu Wakati wa mafunzo haya yanayoendelea katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotel mjini Mtwara leo, mmoja wa wanasemina Sarah Machumu ambaye pia ni Afisa usimamizi wa fedha Ofisi ya Mkuu wa mkoa Dar es Salaam anasema mfumo wa zamani unaotumika hadi sasa unachangamoto nyingi ikiwemo kutofanana kwa mfumo kati ya halmashauri moja na nyingine hali ambayo inaleta shida katika ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za pamoja.
Anasema awamu ya tano ya uongozi wa serikali imekuja na utaratibu mpya wa Elimu bila malipo ambapo fedha zinatumwa moja kwa moja kwa watoa huduma hali ambayo inaibua changamoto ya usimamizi na utoaji wa taarifa ya hizo fedha.
Kwa upande wake Mhasibu wa Hospitali ya wilaya ya Rushoto Mwantumu Mbarouk anasema kupitia mfumo unaotumika sasa kumebainika kuwepo na changamoto nyingi hasa kwa watoa huduma. Sababu kubwa ya changamoto hizo ni pamoja na ufahamu mdogo wa masuala ya fedha hali ambayo imekuwa ikisababisha makosa mbalimbali katika utoaji wa taarifa.
Mwantumu anasema mafunzo haya yamekuja kwa Wakati muafaka hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya tano imekuja na utaratibu wa kutuma fedha moja kwa moja kwa vituo vya utoaji wa huduma zikiwemo shule za msingi na sekondari. Kupitia mafunzo ya mfumo huu mpya itasaidia kupata njia muafaka ya kusimamia na kuandaa bajeti ya mapato na matumizi ya fedha hizo na hata kuyatolea taarifa.
Awali akifungua mafunzo haya yanayofanyika katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotel mjini Mtwara leo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Elias Nyabusani anasema mafunzo haya yatasaidia kuondoa kasoro nyingi zikiwemo zile za ukaguzi. Anasema baadhi ya kasoro za ukaguzi wa fedha zilikuwa zikitokana na mapungufu ya kimfumo hasa katika suala la kurekodi na kutoa taarifa za mapato na matumizi ya fedha. Anasema katika kipindi hiki ambacho maendeleo ya kiteknolojia yamekuwa hasa katika matumizi ya simu mafunzo haya yatasaidia kuzisogeza taarifa za kiganjani. Amesisitiza watendaji kuwa makini katika kuhakikisha wanayatumia mafunzo haya kutatua changamoto zinazowakabili.
Akielezea malengo ya mafunzo haya mtaalamu wa mifumo ya TEHAMA na Mawasiliano kutoka mradi wa PS3 Desideri Joseph Wengaa anasema mafunzo haya ambayo yanatambulika kwa lugha ya kiingereza kama ‘Fasility Financial Account and Reporting System’ (FFARS) yanalenga kuisaidia serikali kuisimamia masuala ya kifedha kwa vituo vya kutolea huduma, Kama vile zahanati, shule na hospitali kwa lengo la kuhakikisha fedha zinazotolewa zinafanya kazi katika malengo yaliyokusudiwa na kuweka uwazi na uwajibikaji.
Anasema mafunzo haya yanaendeshwa nchi nzima huku kanda ya Mtwara ikiwakutanisha mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Dar es Slaam na Tanga. Amefafanua kuwa mafunzo haya yanatolewa kwa Wahasibu na wasimamizi wa fedha ngazi ya halmashauri na mikoa kwa lengo la kuwawezesha kwenda kuwafundisha watoa huduma ambao wako katika shule, hospitali na zahanati.
video ya tukio zima Bonyeza HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.