Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Byakanwa akisaini Kitabu cha Wageni katika Shule ya Msingi Maendeleo
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Gelasius Gasper Byakanwa amefanya ziara ya kushtukiza kwenye shule za msingi na sekondari Manispaa ya Mtwara Mikindani na kubaini mapungufu ya usimamizi wa shule hizo toka kwa wakuu wa shule.
Shule alizotembelea ni shule ya Sekondari Rahaleo, pamoja na shule Nne za Msingi ambazo ni Shule ya Msingi Maendeleo, Raha Leo, Lilungu na Shule ya Msingi Mivinjeni.
Akiwa ameambatana na Kaimu Afisa Elimu Mkoa, Sallum Masalanga Mheshimiwa Byakanwa amebaini mapungufu ya usimamizi wa Walimu Wakuu wa shule hizo ambayo ni pamoja na Wakuu hao kutokuwa na taarifa za walimu ambao hawapo katika eneo la kazi kwa sababu mbalimbali wakiwemo wenye likizo za ujauzito. Pia walimu kutofuata taratibu za kiutumishi wanapoomba ruhusa ya kwenda nje ya kituo cha kazi.
Mapungufu mengine ni walimu wakuu kutopanga mikakati na walimu wao juu ya kuongeza ufaulu jambo aliloliagiza katika kikao na wadau wa elimu kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu. Aidha walimu hao wameshindwa kutimiza agizo alilolitoa kwenye kikao cha wadau wa elimu ambapo aliagiza kubandikwa majina ya wanafunzi walio faulu mitihani ya taifa mwaka 2017 na walimu waliowezesha wanafunzi hao kufaulu.
Kufuatia hali hiyo Mheshimiwa Byakanwa amemuagiza Kaimu Afisa Elimu Mkoa Salum Masalanga ampatie maelezo juu ya walimu ambao hakuwakuta kazini.
Huu ni mwendelezo wa utaratibu aliojiwekea Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha ufauru kwa wanafunzi mkoani Mtwara unabadilika.
Katika matokeo ya kidato cha pili yaliyotangazwa hivi karibuni mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya 26 kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Kufuatia matokeo hayo yasiyorodhisha Mheshimwia Mkuu wa Mkoa alifanya kikao na wadau wa elimu na kupeana mikakati ya kuhakikisha hali ya ufaulu inabadilika ambapo wadau hao waliwekeana mikakati ambayo anafuatilia utekelezaji wake..
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.