Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala leo tarehe 13 Desemba 2024 amekabidhi magari matano na pikipiki tisa kwa Halmashauri za Mkoa wa Mtwara yaliyotolewa na Serikali kwaajili ya kuboresha huduma za chanjo.
Kanali Sawala amewatoa hofu Halmashauri Wilaya ya Newala ambayo bado haijapata gari la usimamizi wa chanjo kuwa hawajasahaulika kwani ugawaji wa vifaa unaendelea na mkoa unazidi kupokea. Aidha amewataka viongozi wa halmashauri hiyo kuendeleza mahusiano na idara zingine pamoja na halmashauri zingine ili huduma za chanjo zisikwame kwasababu ya kutokuwa na gari la usimamizi wa chanjo.
“Kipekee sana niwaombe viongozi na waendeshaji wa vyombo hivi kuzingatia matumizi sahihi ya vyombo hivi sambamba na kuvifanyia matengezo kinga ya kawaida pamoja na matengenezo makubwa kwa wakati ili viendelee kusaidia katika shughuli za chanjo kwa muda mrefu kama ilivyo adhma ya Serikali yetu. Alieleza Kanali Sawala.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bi. Nanjiva Nzunda alieleza “Ni imani yangu vyombo hivi vitaongeza kasi ya kusimamia huduma za chanjo zinazotolewa katika halmashauri kupitia vituo 287 hatimae kufikia walengwa 70,561 katika mkoa.”
Katika hafla ya mgao wa magari na pikipiki za usimamizi wa huduma ya chanjo yaliyokabidhiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapema Desemba 2024, Mhe. Philip Mpango, Mkoa wa Mtwara ulipata Lori aina ya Isuzu NMR85H yenye thamani ya Dola za kimarekani 37,135 kuiwezesha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kusambaza chanjo kwenye Halmashauri.
Aidha, Mkoa ulipokea Magari manne aina ya Toyota Hilux Double cabin yenye thamani ya Dola za kimarekani 180,092 ambayo yamekabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya Mtwara, Masasi Mji, Nanyamba Mji na Newal Mji hivyo kufanya Halmashauri 8 za mkoa wa Mtwara kuwa na magari ya usimamizi wa chanjo. Pikipiki tisa zenye thamani ya Dolar za kimareni 13,305.43 zagaiwa kwa kila Halmashauri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.