Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala amewataka wafanyakazi kufanya kazi bila kubagua huku akiwataka kutoa huduma nzuri kwa wananchi wanaowahudumia. Amezungumza hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani yaliyofanyika mapema leo tarehe 01 Mei 2025 katika viwanja vya Sabasaba wilayani Newala.
Kanali Sawala pia amewataka waajiri na wafanyakazi kushirikiana huku akiwataka waajiri kutoa mikataba inayofuata sheria ili wasiwe na migogoro katika sehemu zao za kazi na kuleta maendeleo.
“Naagiza kila Taasisi kuanzisha mabaraza ya wafanyakazi ambayo yatajadili na kushughulikia changamoto za watumishi kazini.” amesema Kanali Sawala.
Katika hatua nyingine, Kanali Sawala ametoa rai kwa wafanyakazi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 huku akiwasisitiza kuchagua viongozi bora.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, CPA. Bahati Geuzye, ametoa wito kwa wafanyakazi kuipenda Mtwara na kuacha tabia ya kutafuta uhamisho kila mara huku akisisitiza kuwa kuhama sio suluhisho la kila changamoto.
Maadhimisho hayo yameambatana na ugawaji wa vyeti na zawadi Kwa wafanyakazi bora wa mwaka katika kila idara kutoka Halmashari na wilaya zote za Mkoa wa Mtwara.
Kitaifa maadhimisho hayo yamefanyika mkoa wa Singida yakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo ametangaza kuwa Serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa 35% kutoka Shilingi 370,000/= hadi kufikia 500,000/= kuanzia mwezi Julai 2025.
Kauli mbiu iliyobeba maadhimisho hayo ni “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee Viongozi wanaojali hali na maslahi ya wafanyakazi, Sote tushiriki.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.