Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wametambulisha mpango mpya unaolenga kusajili na kutoa vyeti vya watoto chini ya miaka mitano kwa mikoa ya Lindi na Mtwara. Mpango huu unaotarajiwa kutolewa bila malipo umetambulishwa jana kwa viongozi wa Mkoa wa Mtwara katika ukumbi wa Boma Mkoa ulioko Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara.
Akiwasilisha mpango huo, Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson amesema Kupitia Mpango huo watoto watasajiliwa na kupata vyeti hapo hapo bila malipo katika vituo vya Tiba na Ofisi za Watendaji Kata tofauti na awali ambapo iliwabidi kwenda katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Aidha, Mpango huu utaweza kurekebisha mapungufu mengi ya mfumo wa usajili uliopo ambayo yalisababisha wazazi na walezi wengi kushindwa kuwasajili watoto na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Amesema licha ya changamoto kwa wazazi serikali pia imekuwa ikikutana na changamoto ya kukosa takwimu sahihi na muhimu kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya Taifa kama vile Afya, elimu na maendeleo ya jamii ambazo hutumika kama viashiria vya Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals).
Amesema Takwimu za Sensa ya Mwaka 2012, zinaonesha ukubwa wa tatizo ambapo ni asilimia 13.4 tu ya wananchi wa Tanzania Bara walionekana kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa na hivyo Tanzania kuwa moja ya nchi zenye kiwango cha chini sana cha usajili barani Afrika.
‘Hii ni changamoto ambayo Serikali kupitia RITA, kama Taasisi yenye dhamana ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu ikiwemo Vizazi, pamoja na wadau wengine wa usajili wameona ni muhimu kuchukua hatua stahiki kwa kuanzisha Mkakati wenye lengo la kukabiliana na hali hii’. Amesema’.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego amesema mpango huu utasadia kwa kiasi kikubwa kupambana na tatizo la Takwimu katika mkoa wa Mtwara. Amesema watoto waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa katika Mkoa wa Mtwara ni asilimia 9.4 tu hivyo kilichobaki ni viongozi kuamua kuleta mabadiliko?
Aidha Mheshimiwa Dendego amewashukuru RITA kuamua kufanya uzinduzi wa mpango huo mkoani Mtwara na hivyo kuwaelekeza uzinduzi huo ufanyike wilayani Tandahimba septemba 26 mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.