Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Evod Mmanda (Mwenye suti Nyeusi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa safari za meli ya biashara kutoka Mtwara hadi Moroni Comoro
Chemba ya Wafanya biashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) wamezindua Meli ya Biashara itakayokuwa ikifanya safari zake kati ya Mji wa Mtwara, Tanzania hadi mjini Moroni nchini Comoro. Zoezi hilo limefanyika jana katika eneo la bandari ndogo iliyoko karibu na hotel ya Southern Cross zamani ikiitwa Msemo Hotel mjini Mtwara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ambao utaanza na meli ya VILLE DE FOMBONI MOH 0022, Mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Mtwara Swallah Said Swallah amesema kupatikana kwa usafiri huo ni suala ambalo wamelipigania kwa muda mrefu ikiwani hatua muhimu ya kuunganisha wafanyabiashara wa mkoa wa Mtwara na wale wa Comoro.
Amesema ziko sababu nyingi muhimu za kuruhusu biashara hiyo hasa kutokana na jiografia ya maeneo haya mawili. Amesema umbali kutoka Mtwara hadi Comoro ni kilomita 321 wakati nchi zingine ambazo zimekuwa zikifanya biashara na Comoro ni kilomita zaidi ya 3000.
Amesema hadi mwaka 2016 Tanzania ambayo ndiyo kijiografia iko karibu zaidi na Comoro ilikuwa ni ya 17 kati ya nchi ambazo zimekuwa zikifanya biashara na nchi hiyo. Amezitaja nchi ambazo zimetawala soko hilo kuwa ni pamoja na Ufaransa, Afrika Kusini, Nchi za Kiarabu, Madagasca na nchi zingine. Amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuchangamukia fursa hiyo ili kujiongezea kipato.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi wa ufunguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda ambaye alikuwa akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego amesema kuna kila sababu ya Mkoa wa Mtwara kunufaika na biashara hiyo kwani hakuna bidhaa ambazo zinahitajika Comoro ambazo hazipatikanani Mtwara. Amesema mahitaji makubwa ya Comoro ni pamoja na mazao ya vyakaula kama Nafaka, Magimbi, Viazi mbogamboga ambavyo vyote kwa pamoja vinapatikana Mtwara.
Mheshimiwa Mmanda amewataka wananchi wa Mtwara kuchangamukia fursa badala ya kukaa wakaendelea kulalamika hatimaye soko hilo kutawaliwa na watu wa nje ya mkoa.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakifanya biashara na nchi hiyo wamesema biashara ya bidhaa kutoka Tanzania kwenda Comoro inalipa.
Mfanyabiashara wa mbogamboga, Lukia Liyumba amesema vyakula kama mboga za majani na viungo vinahitajika sana huko Comoro. Ametolea mfano kuwa nyanya ambazo hapa Mtwara zinaweza kununuliwa kwa shilingi 500, mjini moroni zinauzwa shilingi 2000.
Aidha Mwajuma Athumani anasema amekuwa akipeleka korosho ambazo anazinunua hapa mjini Mtwara kwa shilingi 20,000 kwa kilo lakini mjini Comoro bidhaa hiyo huuzwa hadi shilingi elfu arobaini. Amewataka wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuchangamukia fursa ya biashara hiyo.
Kutazama video ya tukio hili bonyeza HAPA
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.