Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa ukitembelea Kituo cha kuzalisha Umeme kwa ajili ya kiwanda cha saruji cha Dangote wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Juni 18, 2018
Bei ya saruji inayozalishwa na kiwanda cha Dangote inatarajiwa kupungua mara baada ya kuanza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia. Aidha, ajira zitaongezeka hali itakayosaidia kuongeza pato la wananchi. Hayo yamesemwa jana kupitia taarifa ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme unaotokana na gesi asilia kwa ajili ya Kiwanda hicho.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2018, Fundi Sanifu wa Mradi huo, Walter Nyaki amesema mradi huo ambao uko katika hatua ya mwisho ya usimikaji wa mitambo utawezesha uzalishaji kuongezeka na hivyo bei kupungua wakati ajira ikiongezeka.
‘Mradi huu ukikamilika utawezesha kiwanda cha Dangote kuongeza uzalishaji kwa asilimia 400 na kupunguza gharama za uzalishaji kwa asilimia 90 ambapo itapelekea kuongezeka kwa vijana wanaoajiliwa katika Kiwanda'.
Pia, kwa kuwa gharama za uendeshaji zitapungua itasaidia kupungua kwa bei ya saruji hali itakayopelekea wananchi kumudu kununua saruji hiyo na kuwa na makazi bora. Pia kurahisisha ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari’. Amesema Nyaki.
Kwa Upande wake kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2018, Charles Francis Kabeho aliyeongoza timu ya wakimbiza mwenge kukagua Maendeleo ya mradi huo ameshukuru uongozi wa kiwanda cha Dangote kwa kuamua kuwekeza Tanzania na kuwataka wananchi kuchangamukia fursa zinazotokana na uwepo wa kiwanda hicho.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mheshimiwa Evod Mmanda amesema matarajio ya Wilaya kwa kiwanda hicho ni makubwa kwani kinasaidia kuongeza mapato ya mtu mmoja mmoja na halmashauri kwa ujumla. Pia kiwanda hicho kinasaidia kuitangaza Mtwara katika jumuia ya Kimataifa. Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa muwekezaji huyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.