Waziri wa Biashara, Viwanda na uwekezaji Mhe. Dkt Ashatu Kijaji amefanya ziara ya siku moja ndani ya mkoa wa Mtwara siku ya tarehe 07 Januari, akiambatana naibu waziri wa madini Mhe. Dkt Steven Kiruswa lengo likiwa ni kukakugua maeneo yote ya uwekezaji na kutatua migogoro.
Halikadhalika katika ziara hiyo Dkt. Kijaji ametembelea kiwanda cha sukari cha S.J sugar pamoja na kiwanda cha chumvi na baadhi mashamba ya chumvi kisha kupata nafasi yakuongea na wazalishaji wa chumvi na kusikiliza kero zao.
Akitoa maelekezo ya Serikali baada ya kukagua eneo la kiwanda cha sukari katika Kata ya Kitele, Halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Dkt. kijaji ametoa miezi 3 ya utekelezaji kwa muwekezaji wa kiwanda hicho.
"Sasa tumepita hapa kwenye alichokiita yeye ni kitalu kwa ajili ya mbegu ili ahamishie kwenda kwenye shamba lake kubwa la miwa, tunaona hapa hakuna kitalu cha mbegu ya miwa ila kuna miwa iliyokauka, kwahiyo huyu bwana ameidanganya Serikali, ninampa miezi mitatu, aanzishe vitalu vingine kwa ajili ya mbegu ili aweze kulitumia vizuri eneo la ekari 4100 alilopewa” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha amemtaka muwekezaji wa S.J sugar kufanya uwekezaji katika kilimo cha miwa kama alivyosema katika mkataba wake kwani lengo la serikali ni kwamba, mpaka kufikia Disemba 2023 taifa letu lisiwe na upungufu wa sukari.
Pia Mhe. Dkt Kijaji ametoa maelekezo ya Serikali kwa wakulima wa chumvi na kuwataka wawe watulivu kwani Serikali inatambua uhaba wa soko la chumvi na wawekezaji nchini na serikali iko tayari kuwasaidia. Amewataka wakulima wa chumvi kuweka takwimu vizuri za uzalishaji wao kwa mwaka ili serikali ijue ni namna gani ya kuwashawishi wawekezaji kuwekeza katika uchakataji wa chumvi ghafi.
"Ndani ya taifa letu hatuna upungufu wa chumvi ghafi, kwa maana hiyo hatuna sababu ya msingi ya kuendelea kuruhusu chumvi ghafi iletwe kutoka nje ya nchi kuja ndani ya taifa letu, tulilifanyia kazi jambo hili kwa mda mrefu ,tumekaa na kama serikali tumekubaliana sasa ni mwisho kwa wale wanaoleta chumvi ghafi kutoka nje, kama analeta chumvi ghafi kutoka nje, awe ameshanunua yote tuliyonayo hapa ndani kwanza" alisema Dkt. Kijaji.
Vilevile ameongeza kuwa Mhe rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameamua kuilea sekta binafsi na hivo yuko tayari kuwasaidia na tarehe 11 Januari kutakuwa na mkutano mkubwa wa kikodi utakaoshirikisha wadau wote wa uwekezaji na viongozi wa serikali.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.