Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita imeweka historia Mkoani Mtwara kwa kuwekeza kiasi cha shilingi bilioni 619.6 kutekeleza miradi ya kimkakati.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo wakati akimkaribisha Katibu Mkuu wa CCM Taifa Mhe. Daniel Chongolo katika Mkutano wa hadhara katika uwanja wa CCM Nangwanda mjini Mtwara na kusema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo katika sekta za Afya, Elimu, Maji, barabara na umeme umeongeza tija katika shughuli za maendeleo na hivyo kuwapunguzia kero wananchi.
"Mhe Katibu Mkuu nikianza kuelezea mafanikio yaliyotokana na uongozi bora wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na CCM nadhani tutakesha, itoshe kusema imeweka rekodi ambayo haitasahaulika kwa Wanamtwara" aliongeza Kanali Abbas.
Pia Kanali Abbas ameishukuru serikali kwa hatua inazochukua kutatua kero za watumishi wa umma hatua ambayo amesema imeongeza hamasa miongoni mwao.
"Mhe Katibu Mkuu katika kipindi Cha miaka miwili tumeshuhidia watumishi 4432 wakipandishwa madaraja na Wakati huo huo serikali ikiajiri watumishi 553 na kuwaleta Mkoani Mtwara" alisisitiza Kanali Abbas.
Aidha Kanali Abbas amemweleza Katibu Mkuu Chongolo kuwa serikali inayoongozwa na CCM kwa kipindi chote imekuwa mstari wa mbele kutatua kero za wakulima wa Mkoa wa Mtwara hususani wanaolima Korosho na kusema kuwa katika msimu huu tayari pembejeo kiasi Cha Tani 10,737,000 zimepokelewa.
Wakati huo huo Kanali Abbas amelitumia jukwaa la Mkutano huo kumweleza Katibu Mkuu kuwa Wanamtwara wanaunga Mkono makubaliano ya Uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam yanayohusisha serikali za Tanzania na Dubai akisisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza tija katika utendaji wa sekta ya Bandari nchini ikiwemo Bandari ya Mtwara.
"Kwa upande wetu sisi Wanamtwara tunaamini mkataba huu utakuwa na manufaa makubwa, sambamba na hilo tunaomba kuanzia Sasa Korosho yetu ianze kusafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara" alisisitiza Kanali Abbas.
Mkutano huo wa hadhara umehudhuriwa na baadhi ya Mawaziri, wakuu wa Mikoa ya Lindi na Ruvuma, viongozi mbalimbali wa Chama pamoja na wanachama wa CCM.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.