Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema uwekezaji unaofanywa na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya maji ni kielelezo cha serikali ya mfano yenye kiu ya kutatua kero za wananchi wake.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika hafla ya utiaji saini mikataba 7 ya miradi mikubwa ya maji itakayotekelezwa katika wilaya za Mtwara na Tandahimba kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 8 na kuongeza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaondoa kero ya maji kwa wakazi wa vijiji vitakavyonufaika na hivyo kuwawezesha kutekeleza shughuli zao za kiuchumi bila kikwazo.
“ Ndugu viongozi na wanahabari mliopo hapa kupitia miradi hii iliyotiwa saini hii leo bila shaka sote tunajionea dhamira ya dhati ya serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo kichwani, tumeishuhudia mikataba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 8 ikisainiwa, cha ajabu utakuta bado kuna baadhi ya watu wanabeza jitihada hizi, jamani hivi hawaoni” alihoji kanali Abbas.
Aidha kanali Abbas pia kupitia jukwaa la hafla hiyo amewaagiza viongozi katika ngazi mbalimbali kuhakikisha wanasimamia kwa karibu miradi hiyo ili iweze kutekelezwa katika viwango vya ubora vinavyoendana na thamani halisi ya fedha iliyotumika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Kanali Patrick Sawala ambaye Wilaya itanufaika na miradi hiyo amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa atashirikiana kikamilifu na watendaji katika ngazi zote ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa tija huku akiwataka wakandarasi waliopewa kazi hiyo kukamilisha kwa wakati.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bi Mwanahamisi Munkunda amemtaka kila mwananchi inakopita miradi hiyo kuwa balozi kwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kutafsiri kwa vitendo dhana ya kumtua mama ndoo.
Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Primy Damas amesema pindi miradi hiyo itakapokamilika itanufaisha wakazi zaidi ya 67,000 katika vijiji 35 vya Wilaya za Mtwara na Tandahimba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.