Katibu Mkuu Wizara ya mambo ya ndani Mhe. Kaspar Mmuya amefanya ziara ya siku moja katika Mkoa wa Mtwara lengo likiwa ni kukagua miradi ya maendeleo ndani ya Jeshi la Uhamiaji. Katika ziara hiyo Katibu Mkuu Mmuya amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed ambapo wamekubaliana kuimarisha mahusiano kati ya serikali ya mkoa, taasisi linazozisimamia pamoja na wadau wote ili kuongeza tija katika miradi inayotekelezwa Mkoani humo.
Katika kikao cha ndani na Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ulinzi na usalama Mhe. Mmuya amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali ya mkoa na taasisi za vyombo vya ulinzi na Usalama hatua ambayo itadumisha mshikamano, umoja na Ari ya kujitoa kudumisha Amani na Usalama hususani katika maeneo ya mpakani ambapo Tanzania inapakana na nchi jirani.
Aidha Katibu Mkuu Mmuya amewataka viongozi wa majeshi wa mkoa, kushirikisha uongozi wa Mkoa katika miradi yote wanayoitekeleza kwa kutoa taarifa sahihi za uzalishaji na utekelezaji wake ili serikali ya Mkoa na wadau wake waweze kushauri au kupendekeza njia Bora inayoweza kuzinufaisha pande zote mbili hatua ambayo pia itasaidia kuchangia kikamilifu kukuza pato la Mkoa.
“Jukumu la ulinzi na usalama ni la kwetu na siyo tu ndani ya Mkoa bali ni kwa Nchi nzima naamini tutafanikiwa tu endapo tutashirikiana kwa karibu katika hatua zote za utekelezaji wa majukumu tuliyopewa, hivyo nawasihi askari wote kwa nafasi zao wakilinde kiapo chao, wasilale, kuhakikisha Nchi yetu iko salama” alisema Mhe. Mmuya.
Pia ameuomba uongozi wa mkoa kuridhia ombi la kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za uhamiaji katika maeneo yaliyopendekezwa ili kuimarisha ulinzi na Usalama.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kutekeleza mradi wenye ofisi nne mpya zilizopo Nanyumbu, Masasi, Newala, na Kilambo ambazo bado hazikidhi mahitaji hasa kwa kanda hii ya kusini ambayo ina changamoto ya kutembelewa na wageni kutoka nchi jirani zinazopakana na Tanzania ikiwemo Msumbiji.
“Mhe. Mkuu wa Mkoa tunashukuru Ofisi zimejengwa lakini hazina nafasi ya kutosha kulingana na Majukumu yetu, hivyo basi nikuombe uzungumze na viongozi wako wa halmashauri muone ni kwa kiasi gani mnaweza kutusaidia kupata eneo kwa ajili ya ofisi kuu” aliongeza Mhe. Mmuya.
Halikadhalika Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amemshukuru Katibu Mkuu kwa uamuzi wake wa kufanya ziara katika Mikoa ya Kusini ambapo amejionea hali halisi ya utekelezaji wa miradi iliyoko chini ya Jeshi la Uhamiaji na kusema kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na Ari kwa watendaji ndani ya jeshi hilo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.