Mwenyekiti wa Bodi ya NDF Mhe. Kitwanga Rashid Ndembo (kulia) akimkabidhi nyaraka za shule mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Joseph Mweda
Shule ya sekondari Kitangali iliyoko wilaya ni Newala mkoani Mtwara imekabidhiwa kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)..
Kufuatia makabidhiano hayo shule hiyo iliyoanzishwa miaka ya 80 inabadilishwa rasmi kuwa chuo cha mafunzo ya ufundi Stadi (VETA) na itaanza kudahili wanafunzi ifikapo Julai mwaka huu.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo jana shuleni hapo Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo Wilaya ya Newala (NDF) ambao ndio wamiliki wa shule hiyo Mhe. Kitwanga Rashid Ndembo amesema wanafunzi wanaoendelea na masomo katika shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha Nne wataendelea na masomo wakati huu ambapo taratibu za kusimika miundombinu ya chuo itakuwa ikiendelea.
Ndembo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilya ya Newala amesema wameamua kuchukua uamzi huo kutokana na mahitaji ya dunia ya sasa inayolenga kupata mafundi stadi.
“kutokana na mabadiliko ya dunia ya sasa ambapo shule nyingi za kata zimejengwa, tumeona kuna umuhimu wa kuwaomba VETA wapokee majengo haya ili yabadilishwe kuwa chuo cha Mafunzo ya Ufundi stadi ambayo ndiyo hitaji kubwa la vijana wengi ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo”
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Joseph Mwanda anasema wanatarajia chuo hicho kuanza kupokea wanafunzi mwezi wa saba mwaka huu na tayari wametenga shilingi milioni 222 kwa ajili ya ukarabati wa awali.
Naye Mwenyekiti Mstaafu wa NDF ambaye pia ni Waziri Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na mbunge wa jimbo la Newala Mjini Mhe. Kapteni George Huruma Mkuchika amepongeza uamuzi huo kwamba unakwenda sambamba na malengo ya serikali kuhakikisha kila wilaya inakuwa na Chuo cha VETA.
“Tungesubiri serikali ifanye kila kitu tungechelewa hivyo sisi tumeisaidia serikali kupata chuo cha VETA wilaya ya Newala” Amesema Mhe. Mkuchika
Shughuli ya makabidhiano ya shule hiyo inayotajwa kuwa na eneo la hekta 48 imefanyika jana shuleni hapo huku ikishuhudiwa na viongozi mbalimbalia wa wilaya hiyo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.