Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amezitaka taasisi zilizopokea mabilioni ya fedha za serikali kwa ajili ya miradi ya kimkakati kusimamia matumizi yake kwa uadilifu ili ubora wake uendane na thamani ya fedha zilizotumika.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo leo mjini Mtwara wakati wa ziara yake ya siku moja ya Kukagua miradi minne ya kimkakati ikiwemo Upanuzi wa Uwanja wa Ndege, Ujenzi wa Chujio la maji katika eneo la Mangamba, Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara pamoja na Upanuzi wa Gati la Kuegeshea Meli katika Bandari ya Mwara ambayo kwa pamoja imegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 232.
Akiwa katika uwanja wa ndege wa Mtwara, Kanali Abbas amewaasa viongozi na watumishi kuhakikisha wanasimamia kikamilifu hatua zote za ujenzi wa mradi huo ili kuepuka dosari ambazo zinaweza kuupunguzia sifa ya kuwa moja ya viwanja vyenye hadhi ya kimataifa nchini.
‘’ Ndugu watumishi na viongozi mnaosimamia mradi huu, serikali yetu inayoongozwa na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan inajali sana maendeleo ya wana Mtwara, ndio maana ikaamua kuwekeza shilingi bilioni 56.7 ziweze kuupa hadhi itakayowavutia wadau wa maendeleo kuwekeza Mtwara’’ alisema Kanali Abbas.
‘’ Pindi uwanja huu utakapokamilika ninaamini tutashuhudia ndege kutoka nchi mbalimbali zikitua na kuondoka, nchi kama Msumbiji na Comoro hawa ni majirani zetu, ni vema tukaanza kuangalia namna tutakavyo wahamasisha waufanye uwanja wa Mtwara kuwa kituo chao kikuu cha usafirishaji wa bidhaa’’ aliendelea kusisitiza Kanali Abbas.
Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mtwara Samwel Mruma amesema, tayari wamejiwekea malengo ya kutekeleza miradi kadhaa kama njia ya kuwajengea uwezo wa kujiendesha kibiashara ikiwemo kuweka kituo cha kujaza mafuta kitakacho zivutia ndege za kimataifa kupata huduma hiyo.
‘’Mhe Mkuu wa Mkoa, mimi kama mtendaji mkuu pamoja na timu yangu tutahakikisha tunausimamia mradi huu kikamilifu, siku za nyuma tulikuwa na tatizo la wananchi kuvamia eneo letu lakini baada ya kuweka uzio hali imetulia’’ aliongeza Mruma.
Halikadhalika Mkuu wa Mkoa Kanali Abbas alitembelea Mradi wa Maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA) na kukagua chujio lilogharimu shilingi bilioni 3.4.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja wa MTUWASA Mhandisi Rejea Ng,ondya amesema baada ya kufanya maboresho ya kufunga chujio jipya ufanisi katika uzalishaji maji umeongezeka tofauti na siku za nyuma ambapo walikuwa wakipokea malalamiko mengi kuhusu ubora wa maji waliyokuwa wakizalisha.
‘’ Mhe Mkuu wa Mkoa kwa sasa MTUWASA ina uhakikia wa kuwatosheleza wateja wake kwa kuwapatia maji yenye ubora wa juu, tuna uwezo wa kuzalisha lita milioni 13 kwa siku kama ulivyojionea, lengo ni kuhakikisha thamani ya fedha iliyotumika inaendana na kiwango cha huduma tunayoitoa’’ aliongeza mhandisi Ngóndya.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema ameridhishwa na kiwango kilichofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo na kuiagiza MTUWASA kuweka mikakati endelevu ya kutunza miundombinu ya mradi huo, kutunza mazingira kwa kupanda nyasi na miti sambamba na kuimarisha ulinzi kuepuka uvamizi wa wanachi.
Kisha ziara ya Mkuu wa Mkoa iliendelea katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini ya Mtwara ambapo serikali imetoa shilingi bilioni 15 kukamilisha shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo dokta Jasmine Chilembu alimweleza mkuu wa Mkoa kuwa pindi hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kupokea wagonjwa kati ya 800 – 1000 kwa siku.
Dokta Chilembu aliongeza kuwa kutokana na uchanga wa hospitali hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa watumishi, ukosefu wa nyumba za watumishi, pamoja na kukosa fedha za kutosha za matumizi mengineyo (OC) jambo ambalo amesema linapunguza ufanisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kanali Meja Abbas amewataka watumishi wa hospitali hiyo kuwa na subra wakati serikali inazitafutia ufumbuzi changamoto hizo huku akiahidi kuwasiliana na wizara husika.
Aidha Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema hospitali hiyo itakapokamilika itakuwa mkombozi wa wananchi wa kanda ya kusini hususani wakazi wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma halikadhalika nchi jirani za Comoro na Msumbiji.
‘’Tunataka iwe hospitali ya mfano, tunakoelekea tutaangalia uwezekano wa kutumia teknolojia ya matibabu kwa njia ya mtandao (telemedicine) kama wanavyofanya wenzetu kwenye nchi zilizoendelea, na hapo ndipo tunaweza kusema tumefikia viwango vya juu katika utoaji huduma’’ alisisitiza Kanali Abbas.
Mkuu wa Mkoa alihitimisha ziara yake kwa kutembelea bandari ya Mtwara ambapo amejionea mradi wa upanuzi wa gati la kuegesha meli lenye urefu wa mita 200 uliogharimu shilingi bilioni 157.8.
Akiwa bandarini hapo Kanali Abbas ameutaka uongozi wa bandari hiyo kujiwekea mikakati ya kuwavutia wadau wengi zaidi wahamasike kuitumia bandari hiyo kusafirisha mizigo yao ndani na nje ya nchi.
‘’Fursa za uwekezaji zipo, ninaamini tukizitumia vizuri zitatoa majibu mazuri, nimesikia mmepunguza tozo katika baadhi ya maeneo, huo ni ubunifu mzuri, mimi nawaahidi nitawasiliana na wakuu wa mikoa jirani ili kuhakikisha wanaitumia bandari yetu kusafirisha bidhaa zao’’ aliongeza Kanali Abbas.
Katika ziara hiyo ya siku moja Mkuu wa Mkoa aliambatana na kamati yake ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Mtwara.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.