Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amevitaka vyama vya Ushirika kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji mapato ili yaweze kuchangia kuongeza kasi ya maendeleo.
Kanali Abbas ameyasema hayo katika mkutano wa jukwaa la maendeleo ya ushirika mkoa wa Mtwara kwa mwaka 2023 uliofanyika katika ukumbi wa Polisi Mess na kusisitiza kuwa vyama hivyo vinapaswa kusimamia sekta ya kilimo kikamilifu ili kuboresha maisha ya wakulima.
“Nyinyi kama vyama vya ushirika msipoweka utaratibu mathubuti wa kudhibiti suala la ukusanyaji wa mapato kulingana na matarajio ya mkoa ni dhahiri kwamba sekta ya kilimo na maendeleo ya mkoa yatayumba” alisistiza Kanali Abbas.
Miongoni mwa maagizo ya Mkuu wa Mkoa katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia maadili, kutembelea wanachama, kuendesha vikao na kuandaa taarifa za mapato na matumizi na mipango ya vyama swala ambalo litachangia kurahishisha utatuzi wa changamoto na kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wakulima.
Halikadhalika Kanali Abbas amesisitiza juu ya umuhimu wa matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za kilimo zilizofanyika sambamba na matumizi ya Tehama kwa wanachama wa vyama hivyo ili kuongeza uzalishaji wa mazao.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Hanafi Msabaha amewasihi viongozi wa vyama vya ushirika kudumisha umoja miongoni mwao jambo litakaloongeza ufanisi katika sekta ya kilimo kwa ujumla.
Pia amewataka viongozi hao kwenda kusimamia ubora wa mazao yanayokusanywa kutoka kwa wakulima kama njia ya kuyaongezea thamani katika soko na kuongeza kuwa imebainika kuwa sababu inayochangia kushuka kwa soko la mazao hayo ni udanganyifu unaofanywa na baadhi yao kwa kushirikiana na wakulima wachache wakati wa kupokea mazao kabla ya mnada.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.