Waziri katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George Simbachawene anatarajia kuwaongoza mamia ya wanaKusini na watanzania kwa ujumla katika ufunguzi wa maonesho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane) Kitaifa 2017 inayotarajiwa kufanyika kitaifa katika viwanja vya Ngongo vilivyoko Manispaa ya Lindi Kesho.
Mbali na Mheshimiwa simbachawene, wageni wengine wanaotarajiwa kuwepo hiyo kesho ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Charles Tizeba, Aidha wenyeji wa Maonesho hayo Wakuu wa Mikoa ya Mtwara (Mhe. Halima Dendego) pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi watakuwepo.
Akizungumzia maonesho haya leo baada ya kikao cha maandalizi. Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Zambi amesema kulikuwa na changamoto ya usafi katika baadhi ya maeneo jambo ambalo limeshughulikiwa na sasa kila kitu kiko sawa. Amewataka wadau wote wa kilimo kujitokeza kwa wingi katika maonesho.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego amewasisitiza wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi kutumia fursa hiyo kujifunza namna bora ya kilimo. Amesema maarifa katika kilimo ni njia rahisi ya kumkomboa mwanaKusini kwani ardhi ya kulima ipo, kitu ambacho kimekuwa kikipungua ni maarifa ya kilimo bora.
Maonesho haya yatakayodumu kwa siku 8 yatahitimishwa tarehe 08 Agosti ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Hii itakwua ni mara ya Nne mfululizo kanda ya Kusini inayounganisha mikoa ya Mtwara na Lindi kuandaa maonesho haya kitaifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.