Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego akimkabidhi Mwakilishi wa ITV Mtwara, Lucy Ogutu vielelzo vyake baada ya kunua hisa katika Benki ya TACOBA
Benki ya wananchi wa Tandahimba (TACOBA) imeendelea na Mikakati yake ya kujiimarisha kwa kuuza hisa zake ikiwa ni lengo la kuongeza mtaji. Akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la harambee ya ununuzi wa hisa za Benki hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba jana Meneja Mkuu Benki ya TACOBA Mgwagi Stephen amesema mipango yote ya kuifanya Benki hiyo iwe Benki shindani katika huduma za kibenki hapa nchini imekamilika.
Ameitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha Benki inauza hisa zake ndani na nje ya wilaya ya Tandahimba ikiwa ni lengo la kuifanya iwe Benki ya watu wa kusini hapo baadaye.
Katika harambee hiyo iliyofanikisha ahadi ya shilingi milioni 752 amesema zipo changamoto nyingi zilizojitokeza tangu imeanzishwa lakini uzoefu umewaonesha kwamba hakuna lisilowezekana. Amewataka wananchi wote kuchangamukia hisa hizo zinazouzwa shilingi 1000 kila moja.
Amesema sheria za Tanzania zinataka benki iwe na mtaji unaoanzia bilioni 5 jambo ambalo hawajalifikia. Amesema kwa sasa benki hiyo iliyoanzishwa miaka ya 2000 ina mtaji wa shilingi milioni 999,482. na kwamba mikakati yao ni kufikia malengo katika kipindi kifupi na hatimaye kuwa Benki ya wananchi wote wa ukanda wa Kusini.
Kwa upande wake Mkuu wa Wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego aliyeongoza harambee hiyo amesema mambo yote yanawezekana na kwamba katika mazingira ya uchumi wa Wilaya ya Tandahimba inayoongoza kwa kuzalisha korosho hapa nchini, Bilioni 5 ni kidogo endapo kweli wananchi wa Tandahimba wataamua kuwekeza.
Amesema kuwekeza katika Benki kuna faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu ya mmiliki wa benki hivyo kushiriki katika faida inayopatikana kutokana na Benki hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, Said Msomoka amesema wanatambua umuhimu wa kuwa na Benki hiyo na ndiyo maana halmashauri iliamua kununua hisa na hatimaye kumiliki asilimia 49 ya hisa za Benki hiyo. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2017/2018 wametenga shlingi milioni 600 kwa ajili ya ununuzi wa hisa mpya. Msomaoka amewataka wananchi wa Tandahimba kuchangamukia furasa hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.