Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mheshimiwa Sebastian Walyuba Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tandahimba (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kutokomeza mimba za utotoni.
Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoazimishwa Machi 8 kila mwaka Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mheshimiwa Sebastian Muungano Walyuba amezindua kampeini maalum ya kutokomeza mimba za utotoni. Kampeni hiyo inayoenda kwa kauli mbiu ya ‘Mimi Msichana najitambua, Elimu ndiyo mpango mzima’ inalenga kuzuia vitendo vyote vinavyopelekea kupata ujauzito katika umri mdogo na hivyo kuharibu ndoto za wasichana katika maisha.
Akizindua kampeni hiyo katika zoezi lililofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Tandahimba jana, Mheshimiwa Walyuba amesema ziko changamoto nyingi zinazopelekea kupata ujauzito katika umri mdogo ikiwemo mafundisho ya jando na unyago. Amesema mafundisho hayo ni mazuri pale tu yanapopata miongozo mizuri kwani wako makungwi ambao hutoa mafunzo ambayo hushawishi mtoto kufanya ngono ikiwa ni kufanya majaribio ya kile wanachofundishwa.
Changamoto nyingine ni makubaliano yanayofanywa na wazazi wa pande mbili ili kuharibu ushahidi hasa kutokana na mianya ya kisheria inayoruhusu dhamana kwa mtuhumiwa wa ubakaji. Amesema kuna haja ya kufanya marekebisho ya sheria ili kuzuia dhamana kwa watuhumiwa wa aina hiyo. Hata hivyo ametoa agizo kwa Maafisa Elimu kuhakikisha wanafuatilia kesi zilizoripotiwa mahakamani na kutoa mrejesho kwake.
Awali akiwasilisha taarifa ya wilaya, Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Tandahimba, Hilda Hinju amesema mwaka 2017 jumla ya wanafunzi 55 wa sekondari katika wilaya ya Tandahimba walipata ujauzito. Amezitaja baadhi ya sababu zinazopelekea ujauzito kwa wanafunzi kuwa ni pamoja na tamaduni za makabila ya kusini ikiwemo Jando na Unyago, Uhuru mkubwa wanaopewa watoto toka kwa wazazi wao, unyanyasaji wa kijinsia, na baadhi ya wanafunzi kuishi na Bibi na Babu zao ambao hushindwa kutoa malezi stahili kwa watoto.
Aidha amezitaja baadhi ya athali za mimba za utotoni kuwa ni pamoja na watoto kutofikia malengo yao, magonjwa ya zinaa na matatizo ya kisaikolojia.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Christopher Mushi amesema wamekuja kujumuika na watu wa Tandahimba hasa baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kuonesha kutoridhishwa na hali ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni wilayani Tandahimba wakati wa ziara yake Februali 28, mwaka huu.
Amesema kampeni ya Mimi msichana najitambua, Elimu ndio Mpango mzima ilizinduliwa kwa mara ya kwanza kitaifa mkoani Mara mwaka 2017 na tangu wakati huo kampeini hiyo imekuwa na mwitikio mzuri hivyo wanamatumaini kwamba miaka kadhaa baadaye itazaa matunda. Amesema kwa mwaka jana idadi ya watoto waliopata ujauzito nchi nzima ni wanafunzi 5033 kwa shule za msingi na sekondari huku mkoa wa Katavi ukiongoza kwa asilimia 45, ukifuatiwa na Tabora kwa silimia 43, shinyanga asilimia 41 wakati mkoa wa Mara unashika nafasi ya nne kwa kuwa na asilimia 37.
Kwa upande wake mwanafunzi Seda Michael wa shule ya Msingi Nandonde Wilayani Tandahimba anasema sababu kuu ya ujauzito kwa wanafunzi ni kutotambua hatari ya maamuzi wanayoyafanya. Amesema hali hii ndiyo husababisha matatizo hayo kwani hupelekea kupata ujauzito na hatimaye kujifungua katika mazingira ambayo viungo vinakuwa havijakomaa na hivyo kuathilika kimwili hatimaye kupoteza mwelekeo mzima wa maisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.