Wakati msimu wa kilimo cha korosho 2016/2017 ukielekea mwishoni wananchi wa mkoa wa Mtwara wamepongeza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) kuwa umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mavuno ya korosho. Pongezi hizo wamezitoa jana kwa waratibu wa Mradi huo ngazi ya mkoa Wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani hapa.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Sharifa Asad Kumomonola (56) mkazi wa kijiji cha Mabatini Kata ya Mpapula Wilayani Mtwara anasema msimu wa korosho 2016/2017 alipata shilingi 1,600,000 ambazo zilitokana na utunzaji mzuri wa mikorosho kupitia dawa ya salfa ambayo aliinunua kwa fedha za TASAF.
Sharifa mama wa watoto wawili anasema TASAF imekuwa ikimsaidia shilingi 10,000 kila mwezi na aliamua kujiwekea malengo ya kuzitumia kwa ajili ya kutunza shamba lake lenye mikorosho 69, jambo ambalo limemuwezesha kupata mavuno hayo na hatimaye kuondoa nyasi na kuweka bati kwenye nyumba yake ya vyumba vitatu ambayo imetumia bati 36.
‘Kwa hali duni ya maisha tuliyo nayo tusingeweza kulihudumia shamba hili. Tunashukuru mradi wa TASAF umetuwezesha kulitunza na hatimaye kupata mafanikio haya’. Anaeleza Sharifa.
Licha ya kujenga nyumba hiyo Sharifa anasema vilevile ameweza kununua TV na king’amuzi cha Azam na sasa anaishi na familia yake kwa raha huku akifuatilia kila kinachoendelea duniani kupitia television hiyo.
Anasema wako wanaoziona fedha hizo kuwa ni kidogo lakini hiyo inatokana na kutokuwa na mtazamo wa kujiendeleza. Anasema kama mtu akikaa kwa kutegemea hizo fedha ataziona ndogo lakini kama akiweka mipango ya kuzitumia kuzalisha zingine zaidi atafanikiwa.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa miradi ya TASAF ngazi ya Mkoa, Fatuma Mtanda amempongeza Shalifa na kuwataka watu wengine kuiga mfano huo. Amesema malengo ya mradi wa TASAF siyo kuwapa kila siku ila ni kuwajengea mazingira ya kujifunza na kunyanyuka kutoka hatua moja ya maendele kwenda hatua nyingine hatimaye kujitoa katika kundi la kaya masikini.
Anasema wanaoiona fedha ya TASAF kuwa ndogo na isiyofaa kujiendeleza wanakuwa na mtazamo usio sahihi hivyo wanapaswa kubadilika. Anasema wote waliofanikiwa hawakuanza na mamilioni ya fedha bali walipata kidogo wakakipangilia na kukiendeleza hadi hatua waliyofikia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.