Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mtwara, Swallah Said Swallah ameiomba Serikali kuweka mazingira rafiki ili kuhakikisha korosho zote zinazozalishwa Mtwara na mikoa jirani zinapitia bandari ya Mtwara ili kuiongezea ufanisi katika utendaji kazi wa Bandari.
Ombi hilo amelitoa leo Septemba 25 kwenye kikao kilichowahusisha Mawaziri na Manaibu waziri kwa lengo la kujadili changamoto za wafanyabiashara na wawekezaji wa mkoa wa Mtwara.
Amesema ujenzi unaoendelea katika bandari ya Mtwara ni mkubwa, hivyo ni vema serikali ikafanya maandalizi mapema kwa kumaliza changomoto ambazo zinapelekea bandari hiyo kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
“Ni vizuri tukaweka msimamo sasa jinsi tunavyoweza kuitumia bandari ya Mtwara kikamilifu kwa kuhakikisha korosho zote zinazozalishwa Mtwara na mikoa jirani zinasafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia bandari ya Mtwara ili kuiongezea ufanisi bandari yetu.”
Amesema fursa wanazozikosa wananchi wa mkoa huo kutokana na kuruhusu korosho kusafirishwa kwa barabara kwenda Dar es Salaam ni pamoja na ajira kwa wanamtwara ukosefu wa mapato ambayo yangepatikana kupitia kodi inayotokana na zao hilo.
Kikao hicho cha siku moja kiliwahusisha Mawaziri mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mheshiwa Angela Kairuki, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Innocent Bashungwa pamoja na Waziri wa Madini Mheshimiwa Doto Biteko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.