Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto hatua ambayo amesema itapunguza vitendo vya mmomonyoko wa maadili na hivyo kujenga familia bora zenye upendo zinazotatua matatizo yake kwa njia ya mazungumzo ili kutoa fursa kwa wazazi na watoto kuyapatia ufumbuzi.
Kanali Abbas ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la Siku ya kimataifa ya familia lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Ufundi mjini Mtwara na kusisitiza kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kutambua umuhimu wa familia na mchango wake maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa jambo ambalo litapata tija kwa kuwashirikisha wadau kuanzia nagazi ya familia waweze kujadili na kupanga mikakati ya utekelezaji.
Aidha, Kanali Abbas amewakumbusha wazazi kutekeleza msingi wa malezi hasa kwa kujua na kutimiza majukumu yao ya kuwalinda watoto katika maeneo ya msingi ikiwemo kuwatimizia mahitaji yao ya msingi, kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili sambamba na kuzungumza nao moja kwa moja ili kutambua changamoto zinazo wakabili na maendeleo yao kwa ujumla.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii, Mkoa wa Mtwara Bi Tabitha kilangi amesema kuwa Maadhimisho ya Siku ya familia duniani yanalenga kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na kuiamsha jamii kuhusu umuhimu wa familia ili iweze kuchukua hatua stahiki katika kuimalisha na kuendeleza familia.
Halikadhalika Bi kilangi amewataka washiriki kuitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Maadhimisho hayo inayosema “Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia imara” hatua ambayo itamsukuma kila mwanafamilia kuwajibika kwa nafasi yake ikiwemo kutenga muda wake wa kukaa na familia ikiwa ni pamoja na kuwapatia malezi mema watoto.
Maadhimisho ya Siku ya kimataifa ya familia mkoani Mtwara yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida, wadau kutoka taasisi za kiraia pamoja na viongozi wa dini ambapo wamejadili na kuweka mikakati kuhusu namna ya kuimarisha malezi bora katika ngazi ya familia kama njia ya kuepukana na wimbi la vitendo vya ukiukwaji wa maadili katika jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.