Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC ) limeanza kutekeleza zoezi la kuongeza uelewa kuhusu ukusanyaji wa taarifa za mitetemo katika kitalu cha utafutaji wa Mafuta na Gesi Asili cha Lindi na Mtwara.
Zoezi hilo limetambulishwa rasmi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara leo Augusti 05,2025 katika kikao kilichohudhuriwa na viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea taarifa ya zoezi hilo litakalochukua miezi 18 na kuhusisha vijiji zaidi ya 30 mkoani humo, Kanali Sawala ameeleza kuwa huo ni muendelezo wa mafanikio makubwa yanayoendelea kupigwa na Serikali katika sekta ya nishati nchini.
Kanali Sawala amesema kuwa utekelezaji wa zoezi hilo utaenda sambamba na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo upatikanaji wa ajira za muda mfupi zitakazohusisha uchorongaji wa mashimo na ilinzi wa Vifaa.
“Fursa zingine ni za uuzaji wa bidhaa mbalimbali, utoaji wa huduma muhimu ikiwemo chakula na malazi ambavyo vyote vitawawezesha wananchi kupata na kuongeza kipato”
“Zipo pia faida za kiuchumi ambazo ni matazamio ya baadae ambapo upatikanaji wa mafuta na gesi katika eneo hili utawezesha nchi yetu kuwa na uhakika wa nishati ya mafuta au gesi yatakayotumika ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza mapato ya Serikali” amesema Kanali Sawala.
Kwa upande wake Meneja msaidizi wa mradi huo Mjiolojia Venance Emmanuel, amesema kuwa zoezi hilo linahusisha uchukuaji wa taarifa za mitetemo kisayansi na litahusisha mikoa ya Mtwara na Lindi.
“Lengo kuu ni kukusanya taarifa sahihi na za kina kuhusu muundo wa kijiolojia chini ya ardhi zikazosaidia kutambua maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta nangesi” ameeleza Venance.
Kuhusu taarifa kwa jamii ameeleza kuwa tayari wameshaanza na wanaendelea kukutana na wananchi katika vijiji vyote vinavyopitiwa na zoezi hilo, na kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza na kupata taarifa za kina.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.