M/Kiti wa bodi ya mamlaka ya udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA) Dkt Anthony Diallo amewaagiza viongozi na watendaji katika ngazi za Wilaya na Mkoa kusimamia vema pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali ili ziweze kuongeza tija katika sekta ya kilimo halikadhalika kumkwamua mkulima kiuchumi.
Dkt Diallo ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara ambapo pia aliambatana na baadhi ya wajumbe wa bodi na menejiment ya TFRA na kusisitiza kuwa kila mtu anapaswa kutambua kuwa pembejeo zinazoletwa na serikali zinatokana na kodi ya wananchi hivyo ni vema zikatumika kama ilivyoelekezwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“ Mhe Mkuu wa Mkoa sote tunaona ni kwa kiasi gani Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan amejitoa kumsaidia mkulima wa Tanzania, sasa ni jukumu lenu kuhakikisha mnasimamia kikamilifu zoezi zima la kuwasajili wakulima katika kanzi data ili kupata takwimu sahihi za mahitaji yao ya pembejeo” alisema Dkt Diallo.
“Binafsi nawapongeza sana sekretarieti ya Mkoa kwa kazi kubwa ya kusimamia mchakato mzima wa kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima lakini pamoja na jitihada hizo pia msiyasahau maeneo mengine ikiwemo eneo la udhibiti wa rasilimali za kilimo, tuna taarifa baadhi ya maafisa kilimo wanakiuka matumizi ya pikipiki walizopewa na serikali, inasemekana wengine wanazifanya bodaboda na wengine wanabebea magendo, naomba muwe wakali katika hili” alisisitiza Dkt Diallo.
Pia Dkt Diallo amewaagiza wakuu wa Wilaya ambao ni wenyeviti wa kamati za pembejeo katika maeneo yao kukaa vikao vya mara kwa mara na wakulima na wamiliki wa maduka ya pembejeo ili kupata taarifa za mahitaji na changamoto zao hatua ambayo amesema itapunguza wimbi la migogoro wakati wa zoezi la ugawaji wa pembejeo.
Akijibu hoja za wamiliki wa maduka ya kusambaza pembejeo za ruzuku ikiwemo suala la utofauti wa bei kati ya eneo moja na jingine, tatizo la mtandao pamoja na ukosefu wa takwimu sahihi za wakulima Dkt Diallo amewaagiza viongozi na wataalamu katika ngazi zote kufanya vikao vya mara kwa mara na wamiliki hao hatua ambayo amesema itafungua mlango wa kuzipatia suluhisho changamoto zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abba Ahmed amemhakikishia M/Kiti huyo wa bodi kuwa wataalamu kutoka Sekretarieti ya Mkoa watafanya kila liwezekanalo kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo katika ngazi zote ili kuhakikisha jitihada za Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kumkomboa mkulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo zinapata mafanikio.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.