Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka viongozi wa Mkoa wa Mtwara kuongeza ushawishi katika jamii hasa katika utoaji wa elimu kuhusu mapokeo ya chanjo pamoja na kuongeza uelewa wa jamii ili kuhakikisha mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayozuilika kwa chanjo yanazuiliwa.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo wakati wa akifungua kikao cha kamati ya Afya ya Msingi (PHC) katika ukumbi wa Boma na kusisitiza kuwa Serikali ya Mkoa inafanya jitihada kuhakikisha huduma za chanjo zinawafikia wale wote wenye sifa za kuipata, kama njia ya kukabiliana na magonjwa yanaweza kuzuilika.
Aidha Kanali Abbas amesisitiza kuwa vingozi wanapaswa kuhakikisha wanatumia Kila mbinu kuishawishi jamii kukubali kupata chanjo na kuongeza kuwa endapo itashirikishwa kikamilifu kwa kuwatumia viongozi wa siasa, dini, mila na watu maarufu itarahisisha kufikisha elimu na kuachana na fikra potofu dhidi ya chanjo.
Halikadhalika Kanali Abbas amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, imeweka mpango wa kuwapatia chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi watoto wote wa kike kabla hawajafikisha miaka 14 ili kuwalinda dhidi ya ugonjwa huo ambao kwa sasa ndio unaongoza ukifuatiwa na ugonjwa wa Saratani ya matiti kwa wanawake.
Katika hatua nyingine kikao hicho kimetumika Kutambulisha Mradi wa Girl Effect unaokusudiwa kutoa elimu ya afya ya uzazi sambamba na chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana wanye umri wa miaka 14 katika maeneo mbalimbali Mkoani Mtwara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.