Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhe Daniel Chongolo amesema kazi kubwa ya chama kwa sasa ni kutimiza malengo iliyojiwekea katika ilani yake ikiwemo kutekeleza ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ikiwemo kutatua kero za Wananchi.
Mhe Chongolo ametoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara kwa mikoa ya Kanda ya kusini uliofanyika katika uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona na kusisitiza kuwa miradi ya maendeleo inayogharimu mabilioni ya fedha inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya ukanda huo ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani ya CCM kwa Vitendo.
Aidha Mhe Chongolo amewaeleza maelfu ya wafuasi wa Chama hicho na wakazi wa mji wa Mtwara kuwa CCM haitachoka kuwatumikia na kuwatetea kama ilivyoahidi katika ilani yake huku akitolea Mfano suala la Bandari ambalo amesema limewekwa wazi huku akiwataka Kuwa makini na wapotoshaji wenye nia ovu na Maendeleo ya Watanzania.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi kwa kipindi Cha miaka miwili iliyopita imeweka historia Mkoani Mtwara Kwa kuwekeza kiasi Cha shilingi bilioni 619.6 kutekeleza miradi ya kimkakati.
Kanali Abbas ametoa Kauli hiyo wakati akimkaribisha Katibu Mkuu wa CCM Taifa Mhe Daniel Chongolo katika Mkutano wa hadhara katika uwanja wa CCM Nangwanda mjini Mtwara na kusema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo katika sekta za Afya, Elimu, Maji, barabara na umeme umeongeza tija katika shughuli za maendeleo na hivyo kuwapunguzia kero Wananchi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.