Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed abbas Ahmed amesema kuwa lengo kuu la kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni kukumbusha wajibu wa kila mmoja katika jamii kupigania haki za wanawake hasa katika kutokomeza unyanyasaji unaofanywa na makundi mengine dhidi yao kwani mchango wao ni mkubwa hasa katika ukuaji wa maendeleo.
Kanali Abbas ameyasema hayo katika sherehe ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kimkoa, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Amani, katika Wilaya ya Tandahimba na kusisitiza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika ukuaji wa jamii na uchumi.
“Ni jukumu letu sote kutambua na kuhakikisha kuwa wanawake na wanaume wanaongeza mshikamano na kudumisha usawa ndani ya familia ambako ndiko chimbuko la mambo yote kwani mambo haya yakianzia katika ngazi ya familia itakuwa rahisi jamii kuwa na mtazamo wa pamoja kutambua nafasi ya mawanamke katika usawa” alisema Kanali Abbas.
Aidha kanali Abbas amewataka wananchi wote kuadhimisha siku ya wanawake kwa kutathimini na kutafakari kwa pamoja njisi gani Mkoa umepiga hatua katika kutokomeza changamoto zinawakabili wanawake katika jamii na kuongeza jitihada pale ambapo hawajafanikiwa jambo ambalo litaleta usawa wa kijinsia ambao ni chahu ya maendeleo katika jamii.
Pia amewapongeza wanawake wa Mtwara kwa kujitoa kwao na kuweka mikakati mizuri yenye malengo ya kukuza Mkoa kiuchumi, kijamii, kidiplomasia na kisiasa, na kusema kuwa anaamini kwa ushirikiano waliouonyesha unaenda kuifanya kazi ya kuufungua Mkoa wa Mtwara kuwa rahisi na kuwataka waandae takwimu itakayowaonesha tathimini ya maendeleo yao kila mwaka.
Halikadhalika Kanali Abbas amesema kuwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kuweka mazingira mazuri kwa watoto wa kike kushiriki kikamilifu katika elimu bado tatizo la mimba za utotoni limekuwa kikwazo kikubwa jambo linalopelekea kuathiri afya, elimu na haki ya mtoto wa kike na kumfanya kushindwa kujenga maisha bora ya baadae.
Kanali Abbas amesisitiza kuwa ni jukumu la wananchi wote katika jamii, taasisi zisizo za kiserikali na wadau kwa ujumla kupambana na mimba za utotoni ili kufikia malengo ya kumkomboa mtoto wa kike na kumuwezesha kufikia ndoto zake na Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa mkakati, sheria na sera zinazopinga aina zote za ukatilina kutokuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.