Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Mtwara inashirikiana na mradi wa “USAID Afya yangu” kanda ya kusini na wadau wengine kutoa elimu ya maambukizi ya UKIMWI pamoja na kuwaanzishia dawa wale waliobainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI pamoja na wagonjwa wa kifua kikuu ambapo kwa sasa mpaka Septemba 2024 mkoa wa Mtwara una wagonjwa 35,934 ambao wanatumia dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARV). Aidha ndani ya mwaka mmoja, wagonjwa 1,529 wa kifua kikuu wamepatiwa matibabu.
Kanali Sawala ameeleza hayo mapema leo tarehe 13 Desemba 2024 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utoaji ruzuku wa USAID Afya yangu kwa mwaka 2025 baina ya USAID na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri zote 9 za mkoa wa Mtwara, Hospitali ya Rufaa Mkoa-Ligula, Hospitali ya Rufaa-Ndanda.
Aliongeza kwa kusema kuwa mwaka huu 2024 mpaka Septemba 2025 mradi huu utagharimu jumla ya shilingi Bilioni 3.56 kwaajili ya utekelezaji wa huduma za VVU na kifua kikuu ambapo fedha hizi zitaingizwa moja kwa moja kwenye akaunti za vituo vya kutolea huduma za afya.
“Niwaombe viongozi kusimamia kikamilifu matumizi ya fedha kwa kuzingatia taratibu za kiserikali na masharti ya mkataba mliosaini; kuandaa taarifa ya shughuli zote za utekelezaji wa mradi kwa wakati na kuziwasilisha kwa USAID; kuandaa shughuli na kuomba pesa za shughuli kwa wakati; kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wahusika kwa wakati; kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma vina vifungu stahiki katika mipango yao.” Alisema Kanali Sawala
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.