Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala amepokea hundi ya Shilingi Milioni 100 kutoka Vyama vikuu vya Ushirika vya TANECU na MAMCU kwa ajili ya kuboresha mfuko wa elimu na juma la elimu mkoa wa Mtwara.Kanali Sawala amevipongeza na kuvishukuru vyama vya ushirika kwa kuwahudumia vema wakulima kupitia vyama vya msingi, kuhakikisha pembejeo zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya sita zinawafikia wakulima kwa wakati.
Aidha amewashukuru viongozi wa vyama hivyo vya ushirika kwa kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya na miundombinu katika mkoa wa Mtwara.
“Imeelezwa kuwa ni mwaka wa nne mfululizo tangu 2022 Vyama hivi vinachangia mfuko wa elimu; Mkoa unatumia fedha hizo kuandaa shughuli mbalimbali za kuboresha elimu zenye lengo la kutoa motisha na tuzo kwa Halmashauri, Shule, Walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri; na tumeshuhudia ufaulu wa wanafunzi ukiongezeka. Jambo la kurudisha kwa jamii ni zuri na linapaswa kuigwa kwa vyama vingine.” Alieleza Kanali Sawala
Kwa upande wake Kaimu Mrajisi Msaidizi mkoa wa Mtwara, Ndg. Robert Nsunza ameeleza kuwa kitendo walichofanya Tanecu na Mamcu ni kukamikisha misingi ya Ushirika.
“Msingi wa saba wa Ushirika ni kujali jamii; Vyama vya Ushirika huangalia changamoto zilizopo katika jamii na kutafutia ufumbuzi, vyama vyetu vimeona visaidie sekta ya elimu.” Alieleza Ndg. Nsunza