WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mheshimiwa Charles Mwijage akikagua uzalishaji wa korosho katika Kiwanda cha Kubangua korosho cha CC 2005 kilichoko mjini Mtwara
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mheshimiwa Charles Mwijage ameahidi kuanza mchakato wa kuwawezesha wabanguaji wa ndani kupata korosho. amesema kwa hali ilivyo sasa wabanguaji hawa wamekuwa na changamoto ya kupata korosho kutokana na taratibu za kisheria tulizojiwekea.
Mheshimiwa Mwijage ameyasema hayo leo wakati akikabidhi kwa mkandarasi SUMA JKT eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha wajasiliamali katika eneo la Viwanda vidogo mkoani Mtwara.
Amesema kuwa wabanguaji wa ndani hawapati korosho ghafi za kutosha kuendeleza viwanda vyao kutokana na ugumu uliopo kisheria ambapo pamoja na mambo mengine wanahitaji kuingia katika ushindani na makampuni makubwa.
Amesema musimu wa 2016/2017 Tanzania ilisafirisha tani 320,000 ambapo hitaji la wabanguaji wadogo wa ndani ni tani 240. Amesema hilo halikubaliki hivyo serikali itahakikisha wanapata malighafi na kuendeleza viwanda vyao.
“Tunashindwa kuelewa kuwa tunapotengeneza ajira za hawa akina mama zina tija kuliko kupeleka nje ya nchi… unapotengeneza ajira mtu anakuwa na amani… tumeongozwa na sheria kuliko kutumia sheria.” amesema Mhe. Mwijage
Awali Akitoa taarifa ya shirika hilo Meneja wa shirika la viwanda vidogo vidogo Mkoa wa Mtwara Joel Chidabwa alisema kuwa mkoa wa Mtwara umekuwa na ongezeko kubwa la watu kutokana na ugunduzi wa Gesi asilia na hivyo kumekuwepo na ongezeko la mahitaji ya bidhaa mbalimbali za kutoka viwandani. Amemtaka Mheshimiwa Waziri kusaidia kuondoa changamoto wanazokutana nazo ili wapate nguvu ya kuwandeleza wajasiliamali hao.
“Tunazo zaidi ya hekali 6 ambazo ziko wazi hazijaendelezwa na zinaweza kutumiwa kwa ajili ya viwanda kwa kujenga majengo ambayo yanaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali za viwanda” alisema Chidabwa
Kwa upande wake Mbunge wa Mtwara Vijijini Hawa Ghasia alisema pamoja na mambo mengine kuna tatizo kubwa la umeme na maji mkoani Mtwara hali ambayo inaathiri wawekezaji wadogo kushindwa kufanyakazi ipasavyo.
“Msisema wajasiliamali ni wavivu wanapoingiza bidhaa zao kila baada ya dakika mbili umeme unakatika bidhiaa zinaharibika anapata hasara. Haya mambo lazima yawe na uwiano. Unapoweka kiwanda hakikisha umeme na maji yapo na mtetezi wa haya mambo ni Waziri wa Viwanda na Biashara” amesema Ghasia
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.