Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewataka wadau wa kilimo kuja na suluhisho litakalomsaidia mkulima kuondokana na utamaduni wa kutegemea zao la korosho kama chanzo pekee cha mapato kwani wanaweza kuathirika kiuchumi endapo uzalishaji wake utashuka kama ilivyojitokeza katika msimu wa kilimo 2022/2023.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika kikao cha tathmini ya kilimo ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa BOT mjini Mtwara, ambapo amesema umefika wakati wataalamu na wadau wote wa kilimo watoe majibu sahihi yatakayotoa dira ya kumkomboa mkulima na kuinusuru sekta ya kilimo kwa ujumla,
“Ndugu wajumbe wa kikao hiki, kila mmoja wetu hapa ni shahidi, uzalishaji wa zao letu mama na la kimkakati la Korosho umeathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, halikadhalika mabadiliko ya bei katika soko la dunia” aliwaeleza wajumbe Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
“Sasa hatuwezi kukaa tunalalamika tu, binafsi ninaamini kikao hiki leo kitatoa mwelekeo wa namna tutakavyosimamia kwa tija sekta ya kilimo mkoani kwetu ili kumpa matumaini mkulima shambani asione nguvu zake zinapotea bure” aliongeza kanali Abbas.
Pia Mkuu wa Mkoa Kanali Ahmed Abbas Ahmed amekitumia kikao hicho kuwaeleza wajumbe kuwa mkoa umekuwa ukitegemea mazao ya kimkakati kwa muda mrefu ikiwemo korosho na ufuta, mazao ambayo yamekuwa yakichangia sehemu kubwa ya pato la la mkoa na kuongeza kuwa kuathirika kwa soko na uzalishaji wake hivi karibuni unaulazimu mkoa kukuna kichwa.
“Ndugu wajumbe, nitumie fursa hii kuwaelekeza wataalamu wetu wa kilimo na wadau wote kuwaelimisha wakulima wetu umuhimu wa kulima mazao mchanganyiko ikiwemo ufuta, karanga na mengine, ninaamini kilimo cha aina hiyo kitaongeza tija kwa kuleta matumaini mapya kwa mkulima” alisisitiza Kanali Abbas.
Aidha Kanali Abbas pia amewataka wajumbe na wataalam kutathmini ni kwanini Mkoa umeshindwa kufikia malengo ya kuzalisha tani 240,000 za korosho katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 ili kwa pamoja waweze kuja na maazimio yatakayoleta tija msimu ujao.
Akizungumzia mwenendo wa mauzo ya zao la korosho, Kanali Abbas amesema mpaka kufikia mwezi Januari 2023 tayari ilikuwa imefanyika minada 24 katika maeneo mbalimbali ambapo jumla ya tani 94,000 za korosho ghafi zenye thamani ya Shilingi bilioni 176 tayari zilikuwa zimeuzwa katika Vyama Vikuu vya Ushirika vya TANECU na MAMCU.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa wa Mtwara Alli Linjenje amewaeleza wajumbe kuwa pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kushuka kwa bei katika soko la dunia bado ipo changamoto ya wakulima kukataa kuuza korosho zao katika minada.
“Mheshimiwa Mwenyekiti tumekuwa tukipokea taarifa za wakulima kutoridhishwa na bei na hivyo kubaki nazo nyumbani” alisema Bwana Linjenje.
Linjenje alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kuwaelemisha wakulima ili kuwaepusha kuingia katika utaratibu usio rasmi wa mauzo ya korosho maarufu kama Kangomba.
Naye Mkurugenzi wa bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred ametoa takwimu za uzalishaji na mauzo ya korosho ghafi kupitia chama kikuu cha ushirika TANECU kuwa ni tani 33,062,163 sawa na asilimia 19 zenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 62.
Kwa upande wa chama kikuu cha ushirika cha MAMCU, Bwana Alfred amesema kimeweza kununua tani 59,609,667 za korosho ghafi sawa na asilimia 34 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 111.
Kikao hicho cha siku moja kiliwakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa kilimo kutoka halmashauri za wilaya, Viongozi wa Wilaya na Mkoa, Wenyeviti wa halmashauri, wadau kutoka Vyama Vikuu vya Ushirika pamoja na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.