Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amewahaidi wafanyabiashara na wawekezaji wanaodhamiria kuwekeza upande wa Tanzania hususani katika mkoa wa Mtwara, kuwa serikali ya mkoa tayari imeunda kamati ambayo imepewa jukumu la kubaini changamoto zinazokwamisha biashara kati ya pande hizo mbili ili ziweze kutatuliwa kwa haraka.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo mjini Moron, katika uzinduzi wa maonesho ya kimataifa ya biashara yanayoshirikisha wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali, wengi wao wakitoka Mkoa wa Mtwara Tanzania, ambao kijiografia ndio uko jirani na nchi ya Commoro.
Akizungumza na wafanyabiashara walioshiriki katika katika maonesho hayo katika viwanja vya ubalozi wa Tanzania mjini Moron nchini Commoro, Mhe Abbas amesema kuwa Serikali ya Tanzania kupitia uongozi wa mkoa wa Mtwara tayari umebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara kati ya Commoro na ukanda wa pwani ya kusini hususani mkoa wa Mtwara Tanzania na tayari wameanza kuzifanyia kazi.
"Ndugu zangu mliohudhuria maonesho haya, naomba nichukue fursa hii kuwahakikishia kuwa Tanzania na Commoro mbali na biashara, tuna historia ya muda mrefu, sisi ni ndugu; Kwahiyo uhusiano wetu kibiashara pia unalenga kuimarisha mahusiano yetu kidiplomasia na kiuchumi" aliongeza Kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Aidha Kanali Abbas amesisitiza kuwa kufuatia kamati iliyoundwa na uongozi wa Mkoa wa Mtwara ambao ni mbia mkubwa wa biashara na nchi ya Commoro ilitoa mapendekezo ya kupata meli kubwa itakayopunguza adha ya usafirishaji wa bidhaa za wafanyabiashara kati ya Tanzania na Commoro.
"Naomba nichukue fursa hii kuwahakikishia wafanyabishara kutoka pande zote mbili, kuwa kamati yetu tayari imekuja na mwarobaini wa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zenu kutoka Tanzania kuja Commoro, hivyo naomba mvute subira kidogo mpango huu utakamilika hivi karibuni" alisisitiza Kanali Ahmed Abbas.
Katika maonyesho hayo ambayo pia yalihudhuriwa na balozi wa Tanzania nchini Commoro Mhe. Perreira Silima, Kanali Abbas anatarajia kuongoza mkutano utakaowakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Commoro pamoja na uongozi wa Chemba ya biashara ya nchi hiyo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.