Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala leo tarehe 21 Novemba 2024 katika kikao cha 8 cha Baraza la biashara la Mkoa amezindua zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya kieletroniki kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo vinavyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, wanawake na makundi maalumu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la uzinduzi wa vitambulisho Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Bw. Abdillah Mfinanga alieleza kuwa kwa awamu hii ya kwanza mkoa umepokea jumla ya vitambulisho 502 vya wajasiriamali, ambapo ametoa rai kwa wafanyabiashara ambao hawajajisajili na mauzo yao hayazidi milioni nne kwa mwaka wajisajili ili waweze kufahamika na kufanya biashara kwa uhuru zaidi.
Bi. Judith Pallangyo, Afisa maendeleo ya jamii na mratibu wa kitengo cha masuala mtambuka Halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani ameeleza sifa za wanaotakiwa kupatiwa vitambulisho hivyo, “ni lazima mhusika awe na biashara ndogo ndogo, awe ni mkazi alietambuliwa na uongozi wa mtaa, awe na kitambulisho cha taifa au mpiga kura pia aweze kulipa gharama za usajili ambazo ni shilingi elfu ishirini.”
Akieleza utofauti uliopo kati ya vitambulisho vya sasa na vile vilivyokuwa vikitolewa awali, Bi. Judith alieleza kuwa kitambulisho cha sasa ni cha kieletroniki ambapo taarifa za mhusika zinaingiliana na mamlaka mbalimbali za kiserikali.
Faida za kitambulisho hiko zimeelezwa kuwasaidia kuwatambulisha wajasiriamali kwenye taasisi mbalimbali,kupewa kipaumbele wa maeneo ya kufanyia biashara. Aidha kwa upande wa serikali itasaidia kuandaa bajeti baada ya kufahamu idadi kamili ya wajasiriamali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.