Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed, leo ameungana na mamia ya waombelezaji katika msiba wa mfanyabiashara wa siku nyingi katika soko kuu la Mtwara Marehemu Fakhi Nyambi Luyeye aliyefariki dunia juzi katika hospitali ya Ligula baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akiambatana na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama Kanali Abbas alifika nyumbani kwa marehemu eneo la Sabasaba leo, majira ya mchana na kusema kuwa anafarijika kuwaona wanamtwara wanashirikiana kwa hali na mali katika shida na raha.
“Ndugu waombolezaji, naomba nichukue fursa hii kuwapeni pole kwa msiba huu mzito wa mpendwa wetu, ninaomba mwenyezi Mungu awape subira na hekima hasa katika kipindi hiki kigumu ambacho hakizoeleki kwa binadamu” aliwaeleza waombolezaji Kanali Abbas.
Pia Kanali Ahmed Abbas Ahmed alitumia jukwaa la msiba huo kuwaeleza waombolezaji kuwa mshikamano walionao usiishie wakati wa matatizo pekee bali waendelee kuutekeleza kwa vitendo ikiwemo kushirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
“Ndugu wafiwa na waombolezaji nisingependa kuchukua muda wenu mrefu, lakini naomba mniruhusu niwaeleze kwa ufupi machache kuhusu Mkoa wenu” aliongeza Kanali Abbas.
Kanali Abbas aliwakumbusha waombolezaji kuwa Mkoa wa Mtwara umepata heshima kubwa ya kuzindua mwenge wa uhuru Aprili 2 mwaka huu na kuwataka kushiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi.
Halikadhalika Kanali Abbas ameitumia fursa hiyo kuuarifu umma wa wanamtwara kuhusu ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkoani Mtwara inayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii.
“Mhe Waziri Mkuu ametupa heshima ya kuutembelea mkoa wetu, tunatarajia atatembelea Wilaya na Halmashauri zetu zote, hivyo nawaomba mjitokeze kwa wingi kumlaki popote atakapopita, lakini pia kama kuna jambo au tatizo lolote linalowasibu na mnadhani nina uwezo wa kulitatua niambieni sasa kuliko kumsubiri mgeni” alisisitiza kanali Ahmed Abbas Ahmed.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya wafiwa Alhaji Dadi Mbulu amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuonyesha ukaribu na wananchi na kusema kuwa kitendo hicho ni ishara njema ya viongozi wanaojali watu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Hanafi Msabaha amewahakikishia mamia ya waombolezaji kuwa yuko tayari kushirikiana na Wanamtwara wakati wowote atakapohitajika huku akiwaomba kumpa ushirikiano katika matukio yote ya kitaifa ikiwemo Uzinduzi wa Mwenge na Ziara za viongozi wakuu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.