Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO )kumtembelea na kumuwezesha maarifa zaidi mjasiriamali, Ndg. Abdul Saidi Kichupa anaetengeneza mashine za kubangua korosho, kila moja ikiwa na uwezo uwezo wa kubangua kilo 150 kwa siku.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 08 Agosti 2025 kwenye kilele cha maadhimisho ya Nanenane kanda ya kusini alipotembelea banda la Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba ambapo alielezwa kwa sasa mjasiriamali huyo ameshatengeneza mashine saba.
“Naomba nikutanishwe na huyu mjasiriamali, nimependa anachokifanya. Pia nawaagiza SIDO kumtembelea kumuwezesha, tukiwa na mashine nyingi za wajasiriamali wadogo zenye kubangua kilo 150 kwa siku tutapiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda pia tutaliongezea zao la korosho thamani. Lakini pia nitoe rai apewe kipaumbele kwenye mikopo.” Alieleza Mhe. Jafo
Ndg. Kichupa ni miongoni mwa vijana waliopata ujuzi wa kutengeneza mashine za kubangua korosho kutoka kwa kijana mbunifu, Ndg. Zaidu Mbwana.
Waziri Jafo amezipongeza Halmashauri za Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kutoa mikopo ya 10% kwa wajasiriamali kwa kuzingatia 4% wanawake, 4% vijana na 2% walemavu huku akitoa rai kwa wananchi kupenda kununua vitu vinavyozalishwa na wajasiriamali wazawa ili kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza mbele ya Waziri Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya chakula ili fedha zinazopatikana baada ya kuuza mazao ya biashara zitumike kwa shughuli za maendeleo.
Maonesho ya Nanenane yameambatana na utoaji zawadi kwa washiriki waliofanya vizuri kisekta ambapo Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba imeibuka kidedea kati ya Halmashauri 15 za mikoa ya Mtwara na Lindi zilizofanya vizuri zaidi. Halmashauri ya wilaya ya Tandahimba pia imeng’ara katika washiriki wa jumla ambapo imeshika nafasi ya tatu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.