Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Msongwe Kasekenya tarehe jana 13/08/2024 amefanya ziara mkoani Mtwara kukagua miradi ya ujenzi ikiwemo Barabara ya Mnivata-Masasi km 160 ambayo ni sehemu ya Barabara ya kusini itokayo Mtwara hadi Masasi kupitia Wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala na Masasi.
Barabara hii maarufu kama Barabara ya Uchumi kwani hupita katika maeneo yanayolima kwa wingi zao la Korosho katika Mkoa wa Mtwara inatarajiwa kukamilika tarehe 30/04/2026.
“Lengo la serikali si kujenga barabara halafu iache watu wameumia. Naomba wananchi wafahamu kuwa serikali itatoa fidia kwa wale watakaopitiwa na mradi huu na tayari tathmini ilishafanyika na watu wakalipwa kwa awamu ya kwanza; awamu ya pili tunadaiwa takribani Shilingi Milioni 428 na tayari tumewasilisha maombi Hazina ili pesa ziweze kulipwa.” Alieleza Waziri Kasekenya
Aidha Mhe. Kasekenya aliwataka wakandarasi na pamoja na Mhandisi mshauri kuhakikisha wanatengeza barabara za pembeni ili ziweze kupitika kipindi chote cha ujenzi kwani barabara hiyo ni ya kiuchumi na inaunganisha Halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara huku akisisitiza mradi kukamilika kwa wakati na kwa ubora.
Katika hatua nyingine Mhe. Kasekenya alitembelea eneo la Kilambo ambalo ni mpaka wa nchi ya Tanzania na Msumbiji ambapo serikali inatarajia kujenga daraja ili kuunganisha nchi hizo zinazotenganishwa na mto Ruvuma ili kufungua fursa zaidi kiuchumi.
Bw. Dhulkifu Hamdan, Kaimu Meneja wa TEMESA Mtwara (Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania) alimweleza Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa kivuko cha Mv Kilambo tayari kimemalizika matengenezo kwa sasa wanafanya utaratibu wa kukirejesha mahali hapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.