Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa leo tarehe 19 Novemba 2024 amefanya ziara mkoani Mtwara ambapo ametembelea bandari ya Mtwara na eneo la Kisiwa Mgao itakapojengwa bandari ya kusafirishia mizigo yenye uchafu.
Waziri Mbarawa ameeleza jinsi serikali inavyowekeza kwenye usimamizi wa bandari hususan miundombinu na vitendea kazi. “Mwaka mmoja uliopita bandari ya Mtwara ulikuwa unakuta meli moja kwa siku lakini leo hii nimesimama hapa kuna meli mbili zinapakia zao la korosho. Meli hii inapakia takribani tani 9,000 na meli ile inapakia takribani tani 30,000. Tarehe 21 itakuja meli ya kuleta kifaa kingine ili kuleta ufanisi zaidi wa bandari”
Aidha, Mhe. Mbarawa ametoa rai kwa wafanyakazi kwa bandari kuongeza ufanisi ili meli zikifika bandarini hapo zihudumiwe ndani ya muda mfupi.
Akieleza kuhusu vumbi linalozalishwa ndani ya bandari kutokana na usafirishwaji wa makaa ya mawe, Mhe. Mbawara ameeleza mpango wa serikali wa muda mrefu ambapo itahamisha shughuli zote za usafirishaji na upakuaji wa bidhaa chafu yaani “dust cargo” ikiwemo saruji, mbolea na makaa ya mawe kwenda Kisiwa Mgao ambayo itaanza kujengwa tarehe 03 Januari 2025 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2027 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 434.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri huyo wa Uchukuzi kuzungumza na Waziri wa Kilimo ili mbaazi na ufuta inayolimwa ukanda wa kusini isafirishiwe bandari ya Mtwara.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe. Kanali Patrick Sawala amemuomba Waziri wa Uchukuzi kurejesha safari za shirika la ndege AirTanzania mkoani Mtwara. Nae, Mhe. Mbawara amelipokea ombi hilo na kuahidi miongoni mwa ndege mpya zitakazonunuliwa zitafanyanya safari mkoani hapa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.