Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Halima Dendego akiwasalimia wanafunzi katika moja ya shule za sekondari Mkoani Mtwara wakati wa ziara yake ya kujitambulisha na kukagua ujenzi wa maabara mapema mwaka juzi (picha kutoka Maktaba)
Katika kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Elimu yanayotarajiwa kufanyika kitaifa mkoani Mtwara kuanzia tarehe 24 hadi 28 mwezi huu, wananchi wa mkoa wa Mtwara wameomba nguvu kubwa ielekezwe katika kutatua changamoto za elimu. Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema uamuzi wa serikali kuyaleta maadhimisho hayo kitaifa mkoani Mtwara una lengo jema la kuwafanya wadau wote wa elimu mkoani Mtwara kujitafakari na kuchukua hatua ili kuokoa elimu.
Wamesema kwa muda mrefu mkoa wa Mtwara umekuwa ukitajwa kuwa nyuma kielimu na kwamba changamoto hizo zimekuwa zikitajwa mara kwa mara hivyo maazimishio haya yawe ni sehemu ya kufanya maamuzi ya kuzitatua.
Mmoja wa wananchi hao, Baraka Shadraka mkazi wa mtaa wa Boma Manispaa ya Mtwara Mikindani anasema maeneo mengi ya mkoa wa Mtwara yanachangamoto nyingi ambazo zinahitaji nguvu kutoka kwa viongozi wa serikali. Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na uhaba wa maji, umeme na ubovu wa barabara.
‘Kwa mwalimu mgeni anayetokea Mjini hawezi kuishi kwenye maeno yasiyo na barabara wala maji kama ilivyo huku Mtwara. Serikali inapaswa kuliona hilo na kuweka mikakati ya kuwavutia watumishi wa aina hiyo kufanya kazi katika ameneo hayo.’ anasema
Agness kambuga wa kijiji cha Kitaya wilayani Mtwara yeye analalamikia usimamizi usioridhisha wa walimu katika masuala ya elimu kuwa unapaswa kuangaliwa kwa makini. Anasema kumekuwepo na kutowajibika kwa baadhi ya walimu wakilalamikia ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Anasema mwalimu anapaswa kuwa mbunifu na kutumia maarifa yake kutatua changamoto. Haiwezekani mwalimu akakaa akisubiri aletewe kila kitu.
‘Sisi enzi zetu walimu wetu walikuwa wakitengeneza vifaa vya kujifunzia kutokana na mazingira yaliyokuwa yakiwazunguka. Mfano mwalimu wa Kiswahili alikuwa anaweza kutengeneza moyo wa binadamu kwa kutumia maboksi. Kwa nini walimu wa sasa wanashindwa? Anauliza Agness.
Kwa upande wake Afisa habari Mkoa wa Mtwara Evaristy Masuha anasema maazimisho haya yamekuja Wakati muafaka kwani mkoa umeshaweka mikakati imara ya kuinua elimu.
Anasema mikakati hiyo kwa sasa iko katika utekelezaji hivyo maazimisho haya yatasaidia kushirikishana katika utekelezaji wa maazimio hayo.
Aidha Masuha anakubaliana na wazo la Baraka kuwa moja ya sababu zilizokuwa zikichangia matokeoa mabaya ya wanafunzi mashuleni ni pamoja na mazingira magumu kwa walimu kufanya kazi hasa ikizingatiwa kuwa walimu hao wanatokea mazingira tofauti tofauti. Kupambana na changamoto hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara kupitia kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda wameagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri mkoani Hapa kuhakikisha wanawapokea walimu wapya kwa kuwapa nyumba za kuishi. Aidha kwa wale watakaoshindwa kupewa nyumba halmashauri ihakikishe inawapa usafiri angalau baiskeri kuwawezesha kwenda na kurudi kazini.
Pia halmashauri iwanunulie mahitaji muhimu ya kuanzia maisha kama vile godoro, ndoo, taa za chemli na tochi kwa meneo yasiyo na umeme.
Maazimisho ya Wiki ya Elimu 2017 kitaifa yanaadhmimishwa katika shule ya Sekondari Mangaka iliyoko Wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.