Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar ameilekeza Tasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania (TARI) kituo cha Naliendele kuhakikisha miche wanayowagawia wakulima inazalisha.
Dkt. Omar ametoa maelekezo hayo leo tarehe 23 Februari 2025 katika ziara yake ya siku moja mkoani Mtwara.
“Kilimo kinaajiri zaidi ya 65% ya wananchi. Wenzetu wa bodi ya korosho wameanza kusajili wakulima, TARI na nyinyi muweke mikakati kuhakikisha mnafuatilia ile miche mnayowapa wakulima inaendeleaje, tunataka matokeo chanya.” Alieleza Dkt. Omar
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia pembejeo wakulima jambo lililochochea uzalishaji wa korosho ikiwa ni pamoja na bei nzuri ambayo haijawahi kutokea hapo kabla.
Katika ziara hiyo Dkt. Omar pia alitembelea eneo la Maranje panapojengwa kongani la viwanda zaidi ya 60 ambapo alielezwa zaidi ya maghala 100 yenye uwezo wa kuhifadhi tani elfu kumi yanatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 30, 2025.
Dkt. Omar ametoa rai kwa bodi ya korosho kuongeza jitihada za kuwashirikisha sekta binafsi ili waweze kuwekeza eneo hilo kwani nia ya serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 korosho yote inabanguliwa nchini ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.