Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amewataka wadau wa Kilimo wakiwemo wakulima, watunza maghala na vyama vya ushirika kufanya maandalizi stahiki ya msimu wa korosho Ili kuepuka dosari ambazo zinaweza kuepuka.
Akizungumza wakati wa Ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo wilayani Mtwara, Kanali Sawala amesema baada ya kumalizika salama bila dosari msimu wa ufuta na Mbaazi anatarajia kuona wakulima na wadau wa korosho nao wanasimamia kikamilifu zoezi zima la mavuno, uhifadhi na usafirishaji bila hujuma.
''Ndugu zangu wasafirishaji, watunza maghala na wadau wa Kilimo Kwa ujumla bila shaka Kila mmoja wetu anafahamu tunakabiliwa na msimu mpya wa korosho 2024/25 naomba nendeni mkajipange Ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika Kwa tija'' alisema Kanali Sawala.
Aidha Kanali Patrick Sawala ameongeza kuwa hategemei kuona baadhi ya wakulima wanafanya vitendo vya udanganyifu na kuonya kuwa yeyote atakayebainika hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
''Ndugu zangu wakati tunaingia kwenye msimu wa Korosho naomba tuendelee kuwaelimisha wakulima na wadau wa korosho wahakikishe korosho inayopelekwa ghalani inakidhi viwango vya ubora, sitegemei kupata malalamiko ya korosho chafu'' alisisitiza Mhe Kanali Sawala.
Halikadhalika Kanali Sawala ameitumia ziara hiyo kutoa wito Kwa viongozi katika ngazi zote kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024.
Mkuu wa Mkoa Kanali Patrick Sawala anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya Maendeleo katika halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mji Nanyamba na Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Oct 4, 2024.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.