Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema njia pekee kwa wananchi kuondokana na utapiamlo ni kuzingatia matumizi sahihi ya vyakula bora na kuwa makini na mitindo ya Maisha hatua ambayo amesema itasaidia kujenga miili yenye afya imara itakayolisaidia Taifa kufikia Malengo ya Milenia yatakayochangia kuongeza kasi ya maendeleo katika Nyanja zote.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za Lishe ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Boma mjini Mtwara kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Hanafi Msabaha ambayo imeisisitiza kuwa wataalamu wa Afya na lishe wana nafasi kubwa ya kuwaelimisha wananchi katika ngazi zote kuhusu mbinu za kuepukana na changamoto za utapiamlo na kuongeza kuwa ili kufanikisha lengo hilo kitengo cha lishe chini ya Idara ya Afya kinapaswa kuwapa nafasi wataalamu wake na kuwawezesha kuwasimamia kikamilifu kutekeleza jukumu hilo.
Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya takwimu (NBS) za mwaka 2022 zinathibitisha kuwa Mkoa wetu umefanya kazi kubwa ya kupunguza tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 29.6 kati ya mwaka 2018/2019 hadi asilimia 22 kufikia sasa huku tatizo la uzito mkubwa nalo likipingua kutoka asilimia 4 hadi asilimia 2.
“Pamoja na kupungua kwa baadhi ya viashiria vya utapiamlo, taarifa zinaonesha kuwa bado kuna tatizo la upungufu wa madini joto kwa mujibu wataarifa za tafiti za hivi karibuni, hivyo tunaamini wataalamu wetu wa Afya kwa kushirikiana na mamlaka husika katika eneo hilo watayafanyia kazi matokeo ya tafiti hizo" ilisisitiza hotuba ya Mkuu wa Mkoa iliyowasilishwa na Mhe. Hanafi Msabaha.
Aidha taarifa za tafiti za hivi karibuni zinaonesha kuwa jamii isiyotumia chumvi yenye madini joto ya kutosha ipo hatarini kupata tatizo la upungufu wa madini joto mwilini tatizo linaloweza kusababisha mwathirika kuvimba tezi ya shingo, kuharibika kwa mimba, kuzaliwa kwa watoto njiti pamoja na matatizo ya udumavu wa akili na mwili hali ambayo inatajwa kuathiri uwezo wa watoto kitaaluma” iliongeza hotuba hiyo ya Mkuu wa Mkoa iliyosomwa na Mhe. Msabaha.
Pia hotuba hiyo ya Kanali Abbas imebainisha kuwa Serikali kwa kushirikia na wadau mbalimbali tayari imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la utapiamlo nchini kwa kuhakikisha kuna ongezeko la virutubisho katika vyakula ikiwemo kuhakikisha dosari ya ukosefu wa madini joto kwenye chumvi inadhibitiwa.
Sambamba na hatua hiyo Mkuu wa Mkoa kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mhe Hanafi Msabaha amesema kuwa changamoto nyingine ambazo serikali ya mkoa kupitia wataalamu wake imedhamiria kuzitokomeza ni pamoja na ukosefu wa Vitamin A katika Mafuta ya kupikia, ongezeko la madini ya chuma na foliki ya asidi katika unga wa Ngano na Mahindi, mapungufu ambayo amesema yameanza kufanyi wakazi.
Katika hatua nyingine hotuba hiyo ya Mkuu wa Mkoa imewaelekeza Wakurugenzi watendaji wa Halmashauri zote Mkoani Mtwara kusimama kikamilifu na kuhakikisha chumvi yote inayozalishwa katika maeneo yao inawekwa madini joto halikadhalika vyakula vyote vinavyosambazwa katika shule za bweni hususani vile vinavyohitaji virutubisho vinathibitishwa endapo vimekidhi ubora wa viwango kupitia wazabunini walioteuliwa Ili kuongeza kiwango cha ufaulu na kudumisha Afya za wanafunzi mashuleni.
Naye Afisa Lishe wa Mkoa wa Mtwara Bi. Herieth Kipuyo amesema kuwa Mkoa utahakikisha unashirikiana kikamilifu na wataalamu wa lishe katika halmashauri zote ndani ya Mkoa ili kuzifikisha ujumbe na elimu kuhusu umuhimu wa lishe yenye ubora Elimu ambayo wataalamu watalazimika kuieneza katika ngazi zote huku akiwataka wananchi kuunga mkono jitihada za serikali ya Mkoa za kuondoka na utapiamlo pamoja na udumavu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.