Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jafo amesema kasi ya uwekezaji katika miradi ya kimkakati Mkoani Mtwara ni lazima iende sambamba na utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kama njia ya kuepuka athari za kimazingira.
Waziri Jafo ametoa kauli hiyo leo katika majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo ambapo amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali za kufungua milango kwa wawekezaji hususani katika sekta ya viwanda katika ukanda wa kusini, bado ipo haja kwa mamlaka zinazohusika ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufuatilia kwa karibu ili kujiridhisha namna ambavyo wawekezaji hao wanazingatia sheria mbalimbali za utunzaji wa mazingira.
Akiwa katika bandari ya Mtwara Waziri Jafo ametoa miezi sita (6) kwa uongozi wa bandari hiyo kutekeleza matakwa ya kisheria katika suala zima la usafirishaji na uhifadhi wa makaa ya mawe katika eneo la bandari.
“Kwa kweli nimefarijika sana kuona mnavyopambana kuifanya bandari yenu kuwa lango kuu la kusini, mhe mkuu wa mkoa hongereni sana, na mimi kwa upande wangu nina waagiza wataalamu kutoka NEMC kwa kushirikiana na wataalamu wenu wakae pamoja wafanye tathmini ya kimazingira (Environmental Audit) kama njia ya kujipima na hatimaye tuchukue hatua stahiki’’ alisisitiza Waziri Jafo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Bandari ya Mtwara Norbert Kalembwe amemhakikishia Waziri Jafo kuwa uongozi wa bandari utatekeleza agizo hilo kwa wakati ili kuongeza ufanisi katika suala zima la usafirishaji wa makaa ya mawe.
Katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Mtwara Waziri Jafo pia ametembelea na kukagua dampo la kisasa katika manispaa ya Mtwara Mikindani ambako amejionea utaratibu unaotumika kutupa na kudhibiti taka ngumu.
Akiwa katika eneo hilo, Jafo amepokea taarifa fupi kutoka Afisa Mazingira wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Masumbuko Mtesigwa ambapo amesema mradi huo wenye eneo la ukubwa wa ekeri ishirini na tano (25), mpaka sasa ni ekari tatu (3) tu ndizo zinatumika na kwamba mradi huo unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa rasilimali watu na vitendea kazi ikiwemo magari ya kubebea taka.
Halikadhalika Meneja wa NEMC kanda ya Kusini Boniface Guni amemweleza Waziri Jafo kuwa pamoja na jitihada zilizofanywa na wadau mbalimbali wa mazingira bado suala la matumizi ya plastiki linakwamisha jitihada za uhifadhi wa mazingira.
Kufuatia hali hiyo Waziri Jafo ameiagiza NEMC kufanya msako mkubwa kuwabaini wale wote wanaokiuka sheria hiyo kwa makusudi.
“Serikali imetumia gharama kubwa kujenga dampo hili, hivyo hakikisheni linatumika ipasavyo kulinda mazingira ikiwa ni pamoja na miundombinu yake, lakini pia wale wote wanaokiuka kanuni za matumizi ya dampo hili kama ambavyo nimeshuhudia baadhi yao wakitupa plastiki sheria ichukue mkondo wake” aliongeza Waziri Jafo.
Kuhusu suala la usalama wa eneo la dampo, Waziri Jafo ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuweka alama zinazotenganisha eneo hilo la ekari 25 na makazi ya watu kama njia ya kulilinda lisivamiwe na wananchi.
Waziri Jafo alihitimisha ziara yake katika kiwanda cha simenti cha Dangote ambapo ameupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuchukua hatua madhubuti za kulinda mazingira.
Jafo amesema kuwa siku za nyuma kiwanda hicho kilikuwa kikilalamikiwa na wananchi kwa kukosa miundombinu Madhubuti ya kudhibiti hewa chafu, lakini mara baada ya kuchukua hatua za kudhibiti kero hiyo, hivi sasa hakuna malalamiko.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig Jenerali Marco Gaguti amemweleza Waziri Jafo kuwa mkoa wake ambao umefungua milango mingi ya uwekezaji utahakikisha unasimamia utekelezaji wa sheria za mazingira.
“ Mhe Waziri tumepokea maagizo yako na tutasimamia utekelezaji wake kadri sheria inavyotutaka, sambamba na hilo mhe Waziri, endapo tutabaini kuna eneo ambalo kuna fursa ambayo pengine inatahitaji tathmini ya mazingira mfano kwenye maeneo yenye chemchem ya maji, tutashirikiana na wataalamu wako ili kuhakikisha hatukiuki sheria za mazingira” aliongeza Brig Jenerali Gaguti.
Waziri Jafo pia ameitumia ziara hiyo kuzikumbusha halmashauri zote nchini kutekeleza agizo la kupanda miti Milioni Moja na Nusu (1,500,000).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara
Anuani ya Posta: 544, MTWARA
Simu: +255 23 2333014
Mobile: +255 23 2333014
Barua Pepe: ras@mtwara.go.tz
Haki Miliki © 2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mtwara. Haki zote zimehifadhiwa.